ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 7, 2017

UPELELEZI WAKWAMISHA KESI YAKITILYA.

KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, imeahirishwa hadi Januari 20 mwaka huu kutokana na upelelezi kutokamilika.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi alidai jana katika Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Cyprian Mkeha, hayupo.

Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Hakimu Mashauri alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 20 mwaka huu. Katika shauri lililopita, Hakimu Mfawidhi, Mkeha aliutaka upande wa mashitaka kueleza upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani.

Wakili Esterzia Martin alidai kuwa jalada la kesi hiyo lipo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya kuendelea kuchunguza nyaraka.

Hivyo, aliomba apangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kueleza upelelezi umefikia wapi. Mbali na Kitilya, wengine ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania) mwaka 1996, Shose Sinare na Mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon. Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manane, likiwemo kutakatisha fedha, dola za Marekani milioni sita.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 wa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.