ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 10, 2016

PLUIJM AWAAGA VYEMA YANGA, AMKARIBISHA LWANDAMINA KWA USHINDI WA 2-1.

KOCHA Mholanzi, Hans van der Pluijm leo amewaaga vizuri wana Yanga baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda 2-1 katika m chezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Yanga imalize na pointi 33 nyuma ya Simba SC yenye pointi 35 kileleni baada ya mechi 15 za mzunguko wa kwanza.

Sifa zimuendee kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kwa ushindi wa leo kutokana na kuseti bao la kwanza na kufunga bao la pili.

Lakini Yanga ililazimika kutoka nyuma baada ya Ruvu kutangulia kwa bao la Abrahman Mussa aliyemalizia krosi ya Fully Zulu Maganga dakika ya saba na kumtungua kipa Benno Kakolanya.

Hata hivyo Nahodha wa Yanga leo, Niyonzima akamtoka kwa chenga maridadi kabisa beki Mau Boffu kabla ya kutia krosi iliyounganishwa nyavuni na winga Simon Msuva kuisawazishia Yanga dakika ya 32.

Refa Mathew Akrama wa Mwanza alisindikizwa na Polisi huku akitolewa maneno ya ukali na kocha wa Yanga, Pluijm baada ya kupuliza filimbi ya kukamilisha dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Na haikuwa ajabu refa huyo alipomtoa kwenye benchi Pluijm kabla ya kuanza kipindi cha pili.

Niyonzima aliifungia bao la ushindi Yanga dakika ya 56 kwa shuti la mbali kufuatia mpira uliorudi baada ya shambulizi kali langoni mwa Ruvu.

Yanga wakatulia na kuanza kucheza kwa kupasiana ili kuumiliki mpira kwa lengo la kuwapunguza kasi Ruvu wafanikiwe kuulinda ushindi wao.

Pluijm anaondoka Yanga kumpisha Mzambia, George Lwandamina atakayeanza kazi mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Na Pluijm anaondoka baada ya kuiongoza Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 akicheza jumla ya mechi 128, akishinda 80, kufungwa 23 na sare 25.

Mwaka 2014 aliiongoza Yanga katika mechi 19, akishinda 11, kufungwa mbili na sare sita kabla ya kuondoka kwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo.

Maximo alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.

Na kuanzia Januari mwaka jana, Pluijm ameiongoza Yanga katika mechi 109, akishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.

Na Pluijm anaiachia Yanga mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Ngao ya Jamii na moja Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Katika mchezo wa leo, Pluijm hakuketi kwenye benchi la Yanga, bali alichukua kiti na kuketi pembeni ya benchi hilo kuashiria kwamba anaondoka.

Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Beno Kakolanya, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Andrew Vincent, Thabani Kamusoko, Simoni Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma/Matheo Anthony dk86, Amissi Tambwe na Obrey Chirwa/Juma Mahadhi dk60.

Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Said Madega, Mau Ali Bofu/Yussuf Nguya dk79, Renatus Kisase, Shaibu Nayopa, Jabir Aziz, Abrahman Mussa, Zubeiry Dabi/Raphael Kyala dk60, Issa Kanduru, Fully Maganga/Said Diliunga dk70 na Chande Magoja.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.