ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 29, 2016

UINGEREZA YATOA BIL 6/= KUSAIDIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO.

Moja kati ya athari za tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
RAIS John Magufuli amepokea zaidi ya Sh bilioni sita kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege mbili za Serikali, Rais Magufuli alisema alikabidhiwa fedha hizo jana asubuhi na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke.

Aidha, Rais Magufuli alisema wadau mbalimbali wametoa fedha kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko hilo, lakini Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Amantius Msole pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda, waliamua kufungua akaunti inayofanana na iliyofunguliwa rasmi kwa ajili ya kukusanya fedha za msaada kwa ajili ya waathirika wa tetemeko na kuanza kuzitafuna.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Katibu Tawala huyo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba walikamatwa jana na kufikishwa mahakamani mjini Bukoba.

Kutokana na maelezo ya Rais, baada ya Serikali kuchukua hatua hiyo iliyowapa imani wadau mbalimbali wanaojitolea kuchangia walioathirika na tetemeko hilo, Ubalozi wa Uingereza ulichanga pauni milioni 2.3 zilizotolewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Rais Magufuli alieleza kuwa Uingereza na wadau wengine wamekuwa na imani zaidi kuwa fedha wanazotoa zinawafikia walengwa.

Juzi, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Kagera pamoja na Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ya Bukoba, baada ya viongozi hao kubainika kuwa walifungua akaunti nyingine inayofanana na ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Maafa ya Kagera kwa ajili ya kujipatia fedha.

Viongozi hao wanadaiwa kufungua akaunti yenye jina “Kamati Maafa Kagera” linalofanana na la akaunti rasmi kwa lengo la kujipatia fedha kwa maslahi yao.

Aidha Rais amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei awachukulie hatua watumishi wa benki hiyo walioshirikiana na watumishi hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya benki yenye jina linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa lengo la kujipatia fedha.”

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.