ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 15, 2016

WALIOBEBA COCAINE YA SH 1.5 TRILIONI HATIANI.


By Florence Majani, Mwananchi fmajani@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Watu wawili raia wa Uturuki wamepatikana na hatia ya kuhusika katika usafishaji wa zaidi ya tani tatu za dawa za kulevya aina ya cocaine kwa kutumia meli iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa kwenye ufukwe wa Aberdeen, Scotland mwaka jana.
Mahakama Kuu ya Glasgow, mji mkuu wa Scotland iliwakuta watu hao, Mumin Sahin na Emin Ozmen na hatia ya kukutwa na dawa hizo za daraja A zenye thamani ya Paundi 500 milioni za Uingereza (sawa na Sh1.49 trilioni).
Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo, Kayacan Dalgakiran, Mustafa Guven, Umit Colakel na Ibrahim Dag hawakupatikana na hatia.
Dawa hizo zilizokuwa tani 3.2 aina ya cocaine zilifichwa kwenye meli ya MV Hamal iliyokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania.
Inaaminika kuwa meli hiyo, inayomilikiwa na kampuni ya Kiev Shipping and Trading Corporation, ilitia nanga kwa muda mrefu Guyana, nchi ambayo hutumiwa kupakia cocaine kwa ajili ya kupeleka Amerika Kaskazini na Ulaya.
Taarifa kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini zinaeleza kuwa meli hiyo iliyokamatwa Aprili 23, mwaka huu, ilikuwa imetia nanga maili 100 kutoka ufukwe wa Aberdeen, Uingereza baada ya kuzuiwa kuingia.
Hiyo ni meli ya tatu kukakamatwa ikiwa imebeba mzigo mkubwa wa dawa za kulevya baada ya ile iliyokamatwa Italia ikiwa na usajili wa Tanzania ikiwa na tani 30 za cocaine na nyingine ya Canada iliyokamatwa katika Bahari ya Hindi nchini ikiwa na kilo 283 za cocaine.
Kiwango hicho cha dawa hizo ni kikubwa kuwahi kukamatwa baharini barani Ulaya na usafirishaji huo umeelezewa na maofisa wa polisi kuwa wa utaalamu wa hali ya juu.
Meli hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Istanbul, Uturuki kwenda Tenerife, visiwa vya Canary na baadaye Bahari ya Kaskazi kabla ya kusimamishwa na polisi wa Aprili 23, 2015.
Sahin (47) na Ozmen (51), walipatikana na hatia ya kufahamu kuwa walibeba cocaine kwenye meli yao kati ya Februari 20 na Aprili 23, 2015, na kuhusika kwenye usambazaji wa dawa hizo kati ya Aprili 21 na Aprili 23, 2015.
Jaji Kinclaven, aliyeongoza jopo la majaji 14, alipanga tarehe ya hukumu hiyo kuwa Agosti 12.
Kwa mujibu wa sheria za majini za kimataifa (Territorial Seas/Waters) ilikuwa ni lazima kwa Tanzania kutoa ruhusa kwa mamlaka za Uingereza kuingia katika nyanda hizo za bahari za kimataifa.
“Ilibidi tupate kibali kutoka Tanzania kwa sababu meli hiyo ilikuwa imesajiliwa na inapeperusha bendera ya Tanzania,” inaeleza taarifa hiyo ya Ubalozi.
Kadhalika, taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya Mshauri wa Haki za Kijinai wa Uingereza, Andy Stephen kuomba kibali cha ukaguzi kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, wanausalama wa Uingereza walifanya ukaguzi na kubaini kiasi hicho kikubwa cha dawa za kulevya, kikiwa kimefichwa kwenye boti ndogo ndani ya meli hiyo.
“Baada ya meli kuwasili badarini hapo, ukaguzi ulifanyika kwa siku tatu na wataalamu kutoka kikosi cha mipaka cha Uingereza, wakishirikiana na kitengo cha makosa ya jinai cha Uingereza (NCA) na timu ya mamlaka uchunguzi wa kipolisi ya Scotland, meli hiyo iligundulika kuwa imebeba kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya cocaine,” inasema taarifa ya Ubalozi.
Akizungumzia kukamatwa kwa meli hiyo, Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose amesema kunaonyesha jinsi ulimwengu ulipofikia katika masuala ya usafirishaji wa dawa za kulevya na makosa makubwa ya jinai.
“Kwa kufanya kazi pamoja, ndipo tutaweza kukabiliana na hili. Operesheni ya kuzuia meli hii imefanikisha kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha cocaine,” amesema.
Kadhalika, Melrose amezishukuru mamlaka za Tanzania zilizofanikisha kukamatwa kwa dawa hizo  na kutoa ruhusa kwa vyombo vya usalama vya Uingereza kuzuia uhalifu huu.
Kamishna mstaafu wa Kitengo cha Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema tani 3.2 ni kiasi kikubwa cha dawa hizo ambazo humuathiri mtumiaji yeyote.
“Ni kama ukiumwa mafua, halafu ukatumia cocaine, yanapona hapohapo, lakini ikifika ule muda uliokunywa jana, mafua yanarudi mara tano zaidi ya yale ya jana. Hiyo ndiyo inaitwa alosto,” alisema Kamanda Nzowa.
Mtaalamu wa Kitengo cha Dawa za Kupunguza Uraibu wa Dawa za Kulevya, Dk Ndindi alisema tani 3.2 ni kiasi kikubwa kinachoweza kuwaathiri Watanzania wote kama zikisambazwa.
“Kwa mtu anayetumia gramu moja, huyo ni mtumiaji mkubwa au nguli, kwa hiyo tani 3.2 ni janga,” alisema.
Kadhalika, Dk Ndindi amesema kwa mtu kuathirika na cocaine hutegemea vinasaba, umri, damu na ni mara ngapi ametumia.
“Wapo watu wana vinasaba vya kipekee ambao hata akitumia kiasi gani, haathiriki lakini wengine wakitumia kidogo tu wanapata uraibu,” amesema
CHANZO: MWANANCHI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.