ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, July 19, 2016

WADAU WATOFAUTIANA KASI MPYA NDANI YA CCM.

Dar es Salaam. 
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kukabidhi chama kwa John Magufuli, watu wa kada mbalimbali nchini wameonya kuwa endapo Rais ataingiza staili yake ya utawala, chama hicho kitakuwa hatarini kusambaratika.

Lakini, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuyumba huko kwa chama hicho kikongwe, kutaweza kuyumbisha nchi pia.

Wamesema utaratibu wa kiongozi huyo kuonekana akitoa hatima ya masuala mbalimbali yeye mwenyewe, ni kati ya mambo yanayotarajiwa kuonekana ndani ya CCM mara tu atakapokabidhiwa mikoba.

Wachambuzi hao wanasema ni lazima chama kiwe na utaratibu wa kusikiliza ushauri kutoka kwa makada wake na viongozi wastaafu, badala ya mtu mmoja kuwa mwamuzi wa kila kitu.

Miongoni mwao ni  Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana ambao walipingana na wenzao kwa maelezo kuwa wana imani kubwa Rais Magufuli, ataifanya CCM kuwa moto wa kuotea mbali, huku Dk Bana akienda mbali zaidi na kubainisha kuwa staili ya Rais kupambana na rushwa na ufisadi itakibeba chama hicho.

CCM itafanya Mkutano Mkuu Maalumu Julai 23 mjini Dodoma, ukiwa na ajenda moja tu ya kufanya uchaguzi wa mwenyekiti mpya, ambao ni kama kukamilisha utamaduni wa kumkabidhi Rais Magufuli kijiti cha kuongoza chama kwa kuwa hatarajii kuwa na mpinzani yeyote.

Kikatiba Mkutano Mkuu wa Uchaguzi unatakiwa ufanyike mwakani, lakini CCM imejenga utamaduni wa kumuachia mapema uenyekiti wa chama Rais mpya anayechaguliwa kwa tiketi ya chama hicho.

Kada mkongwe wa CCM, Njelu Kasaka alisema chama hicho kwa sasa hakijajenga mfumo thabiti wa kukiongoza badala yake kimejikita kufuata tabia za mtu mmoja.

“Mimi nawashangaa sana. Wakati nilipokuwa bungeni, tulisema tujenge mfumo wa chama ambao hata aje mtu gani ataendeshwa na mfumo huo tu. Je, akiingia mtu mwenye tabia kama hizi mnafanyaje? Tengenezeni mfumo utakaodhibiti tabia ya mtu yeyote,” alisema Kasaka.

Kuhusu nafasi za uteuzi serikalini, Kasaka, aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Lupa mkoani Mbeya, alisema hakuna shida kuteua mtu unayemwamini, hata hivyo bado kuwe na mfumo wa uongozi.

“Sina shida na uteuzi anaofanya kwa sababu huwezi tu kuteua mtu kwa sababu ni kada wa chama hata kama hana sifa. Nilipokuwa bungeni tulishauri wabunge wasiwe mawaziri ili kumpa nafasi Rais kuteua watu wenye sifa. Walikataa, matokeo yake sasa wanateua wasio na sifa,” alisema Kasaka, mmoja wa wabunge 55 waliowasilisha hoja ya kudai Serikali ya Tanganyika mwaka 1993.

Kasaka alisema mfumo unaojiendesha wa chama ndio unaotakiwa.

“CCM imejengwa kuamini mtu zaidi, ndiyo maana hata zamani ukikikosoa chama unaweza kufukuzwa. Wazungu walitujengea mfumo wa utawala wa Serikali, Bunge na Mahakama. Mhimili mmoja ukikosea, mwingine unakosoa. Ndivyo tunavyotakiwa kuwa katika chama,” alisema Kasaka.

Lakini makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, Pius Msekwa alisema hakuna tatizo lolote miongoni mwa wana-CCM na kwamba anamuunga mkono Rais Magufuli.

“Nani kasema watu wana hofu na Rais Magufuli? Hao ni waongo. Mimi nitajadili nini? Mimi namuunga mkono Rais Magufuli siwezi kusema lolote,” alisema Msekwa.

Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare alisema Rais Magufuli amejenga mfumo wa utawala unaoangalia mtu anayemwamini zaidi, kuliko kuwa kada tu wa chama.

“Kwa kawaida, hivi vyama huwa vinaangalia zaidi ukada wa chama, maadili na misingi vilivyojiwekea. Lakini siku hizi watu hawaangalii sana  hiyo,” alisema.

“Rais Magufuli anakwenda kivyakevyake tu. Anataka awe mtawala mwenyewe. Ndiyo maana hata alivyompata Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alimtoa huko nje na kumwingiza bungeni.”

Mbunge huyo aliyemuangusha Balozi Hamisi Kagasheki (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita, alisema: “Rais anajenga Serikali ya mtu mmoja hata kwenye teuzi zake. Hajali sana chama kinasemaje. Ndiyo maana alipochaguliwa aliendesha Serikali kwa muda fulani bila Baraza la Mawaziri. Alikuwa yeye na Waziri Mkuu tu. Imefika mahali sasa hata Katiba na Sheria alizoapa kuzitii, anaziweka pembeni, anataka mambo ya siasa yafanyike mwaka 2020.”

Hata hivyo, alisema kwa utendaji huo anakihatarisha chama chake na huenda akawapa nguvu wapinzani kupata la kusema kwa wananchi.

“Uongozi huu wa kuweka Katiba pembeni na kuagiza Jeshi la Polisi na vyombo vya dola si mzuri. Ni hatari kwa mfumo wa nchi. Kwa wapinzani tutapata nguvu kwa wananchi,” alisema Lwakatare.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wapinzani wanawaacha CCM wazikane.

“Unajua mimi naamini katika kuwaacha wafu wazike wafu wao. Japo ni ukweli usiopingika kuwa chama hicho ndiyo kinachoongoza Serikali, ni dhahiri kuwa CCM ikiyumba, Serikali itayumba na nchi itaingia kwenye mtikisiko,” alisema Mbowe.

“Huo ndio ukweli ambao huwezi kuupinga. Kwa hiyo stability ndani ya CCM ina husika kwa kila mtu mwenye akili timamu. Lakini nani anapewa uenyekiti, hayo tutawaacha wafu wazike wafu wao,” aliongeza Mbowe.

Alisema hoja yao kama wapinzani ni mfumo mzima wa uongozi, akisema kumekuwa na ukandamizwaji wa demokrasia ambao CCM inaunyamazia.

“Tumeona Bunge limefanyiwa vurugu, lakini katibu wa CCM hajatoa kauli yoyote. Mwenyekiti hajatoa kauli kwa umma, wanamwachia Rais Magufuli ambaye hajawa mwenyekiti,” alisema.

“Machafuko yaliyotokea Zanzibar, uchaguzi umevurugwa. Bunge la 11 nalo limevurugwa na mambo chungu nzima yanayohusu haki, lakini viongozi wa CCM wenye madaraka wamekaa kimya. Hawachukui hatua.

“(Katibu mkuu wa CCM, Abdulrhman) Kinana amekaa kimya. Kikwete amekaa kimya. Hata uwepo wa Kikwete sioni faida yake, uwepo wa (makamu mwenyekiti wa CCM, Philip) Mangula sioni faida yake. Na Kinana sioni faida yake.”

Alisema katika siku za karibuni, viongozi wa CCM wamemwacha Rais Magufuli afanye vitu kama vile hakuna uongozi ndani ya chama hicho.

“Kwa hiyo kilichofanywa na Rais Magufuli kupuuza makada wa chama chake ni ugonjwa wa chama chao, ni uzembe. Wakienda kumkabidhi chama chao hiyo ni juu yao wenyewe. Sisi tunaendelea kupigania demokrasia katika nchi yetu,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema mfumo wa utawala wa Rais Magufuli ni mzuri kwa sababu anapambana na rushwa serikalini. “Rais Magufuli si mkali. Amesema hataki rushwa, hataki maovu. Hao wana-CCM wenye hofu, ndiyo wana makandokando. Wanatakiwa waondoke kwenye chama,” alisema.

“Nimefurahi kusikia Kinana anaondoka, inatakiwa hata Mangula naye apishe. Anahitaji watu energetic (wenye nguvu) watakaomsaidia. Anahitaji watu watakaopambana na upinzani. CCM ilikuwa imechoka, lakini sasa kutakuwa na chama kipya.”

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.