ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, July 7, 2016

MAALIM SEIF YUKO TAYARI KUKAMATWA.




Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kama lina nia ya kumkamata na kumweka ndani lifanye hivyo kwa kuwa yeye yupo nchini. 

Akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Wakfii wa Ngazija mjini Zanzibar, tofauti na jingine lililofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani na kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Maalim Seif alisema nchi inapita katika kipindi kigumu kutokana na dhuluma inayotendwa na watawala dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. 

“Huwezi kuamini kuwa dhuluma hii inatendwa na watawala Waislamu. Hali ni mbaya, wananchi wanapata hilaki kubwa baada ya hao wanaojiita Serikali kubaini kuwa hawakubaliki. 

"Mambo hayo yanafanywa kutokana na kushindwa kuzigeuza nyoyo za wananchi ndiyo maana wanafanya hujuma, vitendo vya kikatili na kuwatisha wananchi,” alisema Maalim Seif. 

Maalim Seif alieleza kusikitishwa na hali ya kamatakamata dhidi ya viongozi mbalimbali wa CUF katika ngazi za wilaya na majimbo na kuwekwa ndani huku wakiteswa, kuadhibiwa na kulazimishwa kukubali kushiriki katika vitendo vya uhalifu ambavyo hawakuvitenda. 

Alibainisha kuwepo mwendelezo wa kauli zinazoashiria azma ya kutaka kumkamata yeye, zinazotolewa na baadhi ya wakuu wa vyombo vya dola. 

“Hakuna haja ya kuwatesa watu, iwapo wanayo azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu wanikamate,” alisema Maalim Seif. 

Maalim Seif alisema vitendo vyote hivyo ni mwendelezo wa dhuluma aliyoitenda Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba 2015 wakati akifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kabla ya kuitisha ule wa marudio wa Machi 20. 

Hii ni mara ya kwanza mpasuko wa kisiasa unawaathiri Wazanzibari hata wakati wa Sikukuu ya Eid -El Fitr inayoadhimishwa baada ya kumalizika mfungo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. 

Akihutumia Baraza lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Dk Shein aliendelea kukazia kuwa Zanzibar haitakuwa na uchaguzi mwingine mpaka mwaka 2020 kwa kuwa Serikali iliyochaguliwa na wananchi imeshaundwa. 

Katika hotuba hiyo ya takriban dakika 35, alisema hakutakuwa na Serikali ya mpito na kueleza kuwa hayo “yanayosemwa mitaani ni maneno ya wababaishaji.” 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.