ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, May 30, 2016

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

TAMKO LA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) KUHUSU SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI
TAREHE 29 MEI, 2016

Ndugu Wananchi;
Tarehe 5 Juni, 2016 Watanzania tutaungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Mazingia Duniani. Kama mnavyofahamu   Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden liliamua kuwa tarehe 5 Juni ya kila mwaka iwe ni Siku ya Mazingira Duniani.

Aidha, Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme (UNEP), lilipitishwa siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka tarehe 5 Juni, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.

Ndugu Wananchi;
Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kutoa fursa kwa jamii duniani kutambua na kuwa na uelewa wa pamoja wa masuala yahusuyo Mazingira; Kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho haya na pia kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda Mazingira; Kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira; Kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na masafi ili sote tufurahie hali hiyo katika maisha yetu.

Ndugu Wananchi;
Kimataifa, mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika nchini Angola. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya nchini Angola ni kutokana na maazimio ya nchi ya Angola ya kupamabana na biashara haramu ya Meno ya Tembo na Pembe za Faru. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya kimataifa ni “Go Wild For Life” Ujumbe huu unahamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti na za makusudi ili kulinda maisha ya wanyamapori kwani wanaunda sehemu muhimu ya mazingira yetu. Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na wadau wengine hapa nchini na kote duniani, wanaendelea na jitihada za kulinda wanyamapori nchini. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameazimia kwamba vita dhidi ujangili lazima tuishinde.
 
Ndugu Wananchi;
Kaulimbiu yetu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira mwaka huu Kitaifa ni Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu.  Maji ni Uhai wa Binadamu, ni Uhai wa Wanyama Pori, na ni Uhai wa Uchumi wa Taifa kwa ujumla. Tumeamua tuwe na kaulimbiu hiyo kutokana uharibifu mkubwa wa Vyanzo vya Maji hapa nchini, kwani sehemu kubwa ya maeneo ya vyanzo vya maji yanatumiwa kwa namna ambazo si endelevu kwa kilimo, uchimbaji madini, ufugaji, ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, mkaa na ujenzi. Hii imepelekea kupungua kwa mtiririko wa maji katika mito mingi nchini takriban kwa kipindi cha miongo mitano iliyopita. Baadhi ya mito imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa sana na mingine kukauka. Tukiendelea na mwenendo huu wa uharibifu wa vyanzo vya maji na mito, mito yetu mikuu hapa nchini, kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha na mingineyo, ambayo inategemewa sana kwa uhai na ustawi wa Watanzania wengi itakauka ndani ya miaka 15 ijayo. Kaulimbiu hii kitaifa inahamasisha jamii kushiriki kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kutofanya shuguli za uharibifu kwenye vyanzo vya maji. Shughuli pekee ambazo tunatakiwa kuzihamasisha ni kupanda miti kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo hivyo na kupiga marufuku shughuli zinazoharibu vyanzo vya maji.
 
Ndugu Wananchi;
Ninatoa wito kwa taasisi zote, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi wote kwa ujumla, kutumia fursa ya maadhimisho haya kushiriki katika kusimamia na kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa ili binadamu na wanyamapori waendelee kuishi.  Tumeelekeza Kamati za Mazingira katika ngazi za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na Wilaya, ambazo Sheria ya Mazingira inaelekeza ziwepo, zianzishwe au zifufuliwe na zichukue nafasi hii ya kutambua na kusimamia vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao na vile    ambavyo vimeharibiwa viongolewe na vihifadhiwe kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu hatutakuwa na maadhimisho ya kitaifa Siku ya Mazingira Duniani, badala yake tumeelekeza Wakuu wa Mikoa kwamba kila Mkoa wafanye maadhimisho haya kwenye maeneo ya Mikoa yao. Tumetoa mwongozo kwa Mikoa kuhusu utekelezaji wa shughuli zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira hususan vyanzo vya maji ambavyo ni muhimu na ni uhai wa kila kiumbe. Kama kawaida yetu, shughuli za maadhimisho ya siku ya mazingira zitaanza tarehe 1 Juni na kumalizika siku ya kilele tarehe 5 Juni, 2016. Siku ya kilele tutakuwa na shughuli mahsusi zitakazoongozwa nami na Makamu wa Rais, Mhe Samia Suluhu Hassan, zitakazoambata na ujumbe maalum unaohusiana na hifadhi ya mazingira. Nitoe wito kwa viongozi wa kisiasa na wa Serikali kwa ngazi zote, viongozi wa dini na taasisi za kijamii na wananchi wote kwa jumla kuwa kila siku katika maisha yetu iwe siku ya mazingira kwa kufanya yafuatayo:
·       Kupanda miti kwenye vyanzo vya maji na maeneo mengine ambayo hali ya hewa inaruhusu kwa sasa;
·       Kuhamasisha kuzuia kufanya shughuli zisizo endelevu  kwenye vyanzo vya maji;
·       Kudhibiti uchomaji moto misitu yetu;
·       Kusafisha visima na vyanzo vingine vya maji;
·       Kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira kwa kutumia sanaa, michezo au vyombo vya habari;
Mapema mwaka huu, Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya tathmini ya hali ya vyanzo vya maji nchini na kutoa mwongozo kwa viongozi wa mikoa kuhusu hifadhi yake.

MASUALA MENGINE YAHUSUYO HIFADHI YA MAZINGIRA

Mkakati Mpya wa Kupanda na Kutunza Miti
Kuanzia mwezi Januari 2016, Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na wadau, na Wizara ya Maliasili na Utalii, imeandaa Mkakati Mpya wa Taifa wa Upandaji na Utunzaji Miti. Mkakati huu ni wa miaka mitano (2016 hadi 2021), unakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 105.2. Katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya mwaka ujao wa fedha, tumetenga shilingi bilioni 2 kama kianzio kwa ajili ya mkakati huu. Tunategemea kwamba baada ya bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha kukamilika, Mfuko wa Taifa wa Mazingira utatengewa vyanzo vya mapato yanayokadiriwa kufikia shilingi bilioni 100, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kifedha ya kugharamia mpango huu na mipango mingine ya hifadhi ya mazingira. Mkakati huu mpya mkubwa umezingatia kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika kampeni za upandaji miti zilizofanyika katika vipindi mbalimbali tangu uhuru wa nchi yetu. Aidha, masuala mengine yatakayozingatiwa katika mpango huu mpya ni uhamasishaji na utoaji wa motisha kwa watumiaji wa nishati mbadala ili kuondoa matumizi ya kuni na mkaa.

Katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Upandaji na Utunzaji wa Miti, kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya na kila taasisi itapewa lengo la upandaji miti. Tutashindanisha shule na vijiji katika upandaji na ukuzaji wa miti  na tutatoa zawadi nono. Maeneo ya wazi ya Serikali yatapandwa miti. Tutarahisisha upatikanaji wa mbegu na miche. Tutashirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhakikisha kwamba Halmashauri zinatunga sheria ndogo (bylaws) za kulazimisha upandaji na utunzaji wa miti. Dhamira yetu ni kuibadilisha Tanzania kuwa ya kijani. Tutahimiza pia mashamba ya miti ya kibiashara kwa watu binafsi.

Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki

Ndugu Wananchi,
Tumefanya uamuzi wa kupiga marufuku moja kwa moja, utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia mwakani (2017).

Mifuko ya plastiki imekuwa ni changamoto kubwa ya mazingira. Kwa sehemu kubwa mifuko hii hutolewa bure na inasambaa, kuchafua mandhari na kuziba mifereji hivyo kusababisha mafuriko na athari nyingine kubwa kwa mazingira. Asilimia kubwa ya uchafu kwenye vyanzo vya maji, kwenye mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.

Ofisi inakamilisha majadiliano ndani ya Serikali na baadaye kuwahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku moja kwa moja matumizi ya mifuko ya plastiki nchini. Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko ya plastiki kujiandaa kuacha shughuli hizo na itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungio mbadala. Tumetuma wataalam wa Serikali katika nchi zilizofanikiwa kwenye jambo hili kujifunza namna bora ya kulitekeleza. Nia ya Serikali ni kuweka zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki ndani ya Sheria. Hii pia inahusu matumizi ya mifuko ya plastiki kufungashia pombe, maarufu kwa jina la viroba.

Natoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko ya plastiki waanze kujiandaa sasa kwa zuio hili. Katika wiki zijazo, Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio hili na taratibu nyingine mahsusi na za kina ili kuepusha mkanganyiko. Hata hivyo, watengenezaji wa mifuko ya plastiki wanaoiuza nje ya Tanzania wataruhusiwa kuendelea kuitengeneza kwa ajili ya soko la nje ya Tanzania.  

Uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira

Ndugu Wananchi,
Kwa muda sasa, kumekuwepo na udhaifu katika uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira. Kwa sehemu kubwa, Sheria ya Mazingira inatekelezwa katika ngazi za Serikali za Mitaa. Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI pamoja na mamlaka nyingine inakamilisha utengenezaji wa Sheria Ndogo za Mazingira pamoja na Kanuni zake ili kuhakikisha kwamba Sheria ya Mazingira inatekelezwa kwa ukamilifu wake. Tutateua Wakaguzi wa Mazingira katika kila Halmashauri na kuzipa nguvu Kamati za Mazingira kutoza faini na adhabu mpya kwa kukiuka Sheria ya Mazingira, ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji.

Vilevile, kwa shughuli za uwekezaji zinazohitaji kufanyiwa Tathmini za Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment), tutawaadhibu wale ambao hawakufanya. Tunatoa muda wa miezi miwili, hadi tarehe 1 Agosti 2016, kwa wale ambao hawana Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira katika shughuli zao waende Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit). Shughuli zinazohusika ni zile ambazo zimeorodheshwa kwenye Sheria ya Mazingira ya 2004, kuanzia kifungu cha 81 - 103 na Kanuni zake za mwaka 2005.

Vilevile, kwa wale ambao hawajalipa tozo za mazingira kwa shughuli zao, tunawapa hadi tarehe 1 Julai wawe wamefanya hivyo. Itakapofika hiyo tarehe na hawajalipa, NEMC italazimika kuzifungia shughuli zao. Shughuli zinazopaswa kulipa tozo ya mazingira zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kifungu cha 230 (2) (b) na Kanuni za Tozo za Mazingira za Mwaka 2008.

HITIMISHO
Ndugu Wananchi;
Nimalizie kwa kusema kwamba hali na mwelekeo wa mazingira ya nchi yetu ni mbaya.  Kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini, asilimia 61 ya nchi yetu inatishiwa kuwa jangwa, ambapo kila mwaka tunapoteza takriban ekari milioni moja za misitu.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira, vyanzo vingi vya maji vimevamiwa na kuharibiwa, mvua zimekuwa hazitabiriki, ukame unaongezeka kwenye maeneo mengi, rutuba ya ardhi imepungua, maporomoko ya ardhi katika maeneo ya milima yameongezeka, mafuriko yanayosomba miundombinu na kuharibu mali na kuchukua maisha ya watu yameongezeka. Kila mvua inapopungua kwa asilimia 10, Pato la Taifa linalotokana na kilimo hupungua kwa asilimia 2. Kila joto linapoongezeka kwa nyuzi joto 2 za sentigredi, mavuno ya mahindi hupungua kwa asilimia 13 na mavuno ya mpunga hupungua kwa asilimia 17.

Uharibifu wa mazingira unaathiri sekta zote nyeti za uchumi na maisha ya Watanzania. Sekta ambazo zimeathirika zaidi ni kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, nishati, huduma ya maji na sekta ya afya. Kwa msingi huo, bila kuwekeza katika hifadhi ya mazingira, jitihada za uwekezaji katika sekta nyingine za kiuchumi na kijamii hazitazaa matunda tunayotarajia. Kwa msingi huo, Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuyaweka masuala ya mazingira kama sehemu ya mhimili wa ajenda ya uchumi na maendeleo ya taifa letu.  

Mwisho, napenda kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya uhamasishaji na ukuzaji weledi kwa wananchi kuhusu Hifadhi ya Mazingira, na hasa katika masuala ya utunzaji wa vyanzo vya maji. Naomba vyombo vya habari viendeleze juhudi hizi za kuelimisha umma kuhusiana na mapambano dhidi ya uharibifu wa vyanzo vya maji. Vyombo vya habari mna nafasi kubwa na naamini mnaweza kusaidia sana katika suala hili.

Nimalizie kwa kuwakumbusha kwamba, suala la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, na utunzaji wa Vyanzo vya Maji ni jukumu letu sote linalotakiwa kufanyika kila siku. Mazingira ni Uhai wa Viumbe akiwemo Binadamu, Wanyama na Mimea; Ni Uhai wa Taifa; na ni Msingi wa Maendeleo Endelevu, hivyo basi tuyatunze kwa pamoja.

January Makamba (MB)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira

29 Mei 2016

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.