ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, May 4, 2016

AZAM FC WAIACHIA RASMI UBINGWA YANGA, WATOA SARE 2-2 NA JKT RUVU CHAMAZI

AZAM FC imepoteza kabisa matumaini ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na JKT Ruvu jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba, Yanga wajitahakikishia kutetea taji hilo Mei 10 wakishinda dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kwani watafikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine ya Ligi Kuu.

Sare hiyo inaifanya Azam FC ijiongezee pointi moja na kufikisha 60 baada ya kucheza mechi 27 na inaweza kumaliza na pointi 69 ikishinda mechi tatu za mwisho, wakati Simba yenye pointi 58 inaweza kumaliza na pointi 70 ikishinda mechi zake nne zilizobaki.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Selemani Kinungai wa Morogoro aliyesaidiwa na washika vibendera Lulu Mushin na Shaffih Mohammed wote wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Mabao hayo yalifungwa na pacha kutoka Ivory Coast, kiungo Kipre Michael Balou dakika ya 31 na mshambuliaji Kipre Herman Tchetche dakika ya 37.

Kipindi cha pili, JKT Ruvu inayofundishwa na gwiji wa soka nchini, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ilibadilika na kufanikiwa kusawazisha mabao yote mawili.
Alianza Mussa Juma kufunga kwa penalti dakika ya 56 na Najim Magulu dakika ya 72.

Kikosi cha Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Abdallah Kheri, David Mwantika/Said Mourad dk46, Himid Mao, Kipre Balou/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk80, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk64, John Bocco na Kipre Tchetche.

JKT Ruvu; Madenge Ramadhani, Hamisi Seif, Omar Kindamba, Paul Mhidze, Renatus Morris, Nashon Naftali, Abdulrahman Mussa/Samuel Kamuntu dk46, Hassan Dilunga, Najim Magulu, Mussa Juma na Saad Kipanga/George Minja dk89.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.