ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, April 25, 2016

AFISA TARAFA ITISO AVUNJA KAMATI YA AFYA YA ZAHANATI YA KIJIJI ATOA WIKI MOJA KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU WA KIJIJI

 Afisa Tarafa wa Itiso Bw. Remidius Emmanuel akimhoji mtendaji wa kijiji cha Zajilwa Bw. Hamisi Mdimu juu ya uhalali wa muhtasari aliouandaa na kuelekezakwa mkurugenzi wa HalmashauriyaChamwino bila kuhusisha Serikali ya kijiji.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji Zajilwa wakiendelea kufuatilia kinachoendelea katika mkutano huo
 Afisa Tarafa akizungumza na wajumbe wa Serikali a kijiji cha Zajilwa mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano na wananchi panija na wananchi wa kijiji hicho

Na Mwandishi Wetu
Akizungumza katika Mkutano na wananchi wa kijiji Zajilwa  wakati akisikiliza Kero za Wananchi juzi, Bw .Remidius Emmanuel ambaye ni Afisa Tarafa  ya Itiso amewataka viongozi wa kijiji hicho kutumia muda mwingi  kusikiliza Kero za Wananchi na kuzitatua, "Nimekwisha toa Maagizo katika Tarafa yangu na pengine nirudie kwa mara nyingine katika kijiji hiki, Viongozi wote tunatakiwa  kupambana na viashiria vya migogoro kabla migogoro yenyewe  kutokea, Kila mgogoro  una chanzo chake . " Jamani  leo unapoona  mawingu lazima ujue hiyo ni dalili ya mvua" Alisema Bw. Remidius 

Kiongozi huyo amesema hayo huku kukiwa na vuguvugu la Wananchi waliowengi  kuonyesha hisia kali za kuipinga Serikali ya kijiji hicho kwa kumtaka Mwenyekiti wa kijiji hicho kuachia ngazi kutokana na wananchi hao kutoridhishwa na utendaji wa Serikali ya Kijiji.

Akizungumza mbele ya Afisa Tarafa  kwa niaba ya Wananchi wenzake Bw. Chacha Marwa amesema  Serikali ya kijiji hicho ni jipu linalotakiwa kutumbuliwa kwa kuwa imeshindwa  kusoma mapato na Matumizi, "hatupati taarifa za miradi inayotekelezwa na Kijiji hiki. Tarehe 21/03/2016 Serikali ilihitisha Mkutano mkuu wa kijiji ambao ulivurugika kutokana na udanganyifu uliojitokeza. Mfano Tulisomewa Mapato ni Tsh 1,645,000 na Matumizi ni Tsh 4,510,000 taarifa inayoonyesha Matumizi kuzidi mapato ya kijiji je fedha nyingine walitoa wapi ? hakuna Umakini katika kuandaa taarifa hizo" Alisema Bw.Chacha huku akishangiliwa na Wananchi wengi na kuongeza  kuwa   "Tunashukuru sana Afisa Tarafa kwa kuja kusikiliza Kero zetu ,hapa kijijini  zipo Kero nyingi sana na Tatizo ni Serikali ya kijiji"

Hata hivyo kwa nyakati tofauti Bw. Remidius Aliwasimamisha  Mwenyekiti wa Kijiji hicho na   Mtendaji wake kujibu  hoja hizo mbele ya Mkutano huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Zajilwa Bw. Athumani  Salum Duda Alikiri kuvunjika kwa Mkutano wa Serikali ya Kijiji wa Tarehe 21/03/2016 nakusema Mkutano huo ulivunjika kutokana na Wananchi kutokubaliana na Taarifa za Mapato na Matumizi, hata hivyo Mwenyekiti huyo akionekana kuwa na kigugumizi alipotakiwa kueleza ni lini sasa Mkutano huo utafanyika.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji hicho Bw. Hamisi Mdimu, Alisema Mkutano huo ulifanyika  na Tayari amekwisha andika Muhitasari hatua iliyopingana na Maelezo  Mwenyekiti wa Kijiji  Bw. Athumani baada ya kusema kuwa  hatambui Muhtasari huo na kwamba hakuna saini yake katika Muhtasari huo , hata hivyo  Wajumbe wa Serikali ya kijiji hicho kwa upande wao walionekana  kushangazwa na Muhitasari huo ambao tayari uliandikwa na  kuelekezwa kwa Mkurugenzi kuonyesha kwamba  Mkutano mkuu ulifanyika  salama kwa kujadili Mapato na Matumizi pasipo kuonyesha kama Mkutano huo ulivunjika.

Akihitimisha hoja hizo Afisa Tarafa Bw.Remidius Emmanuel ,Amesema viongozi wa kijiji hicho ndio chanzo kikubwa  cha Migogoro na  ameangiza ndani ya kipindi cha wiki moja Serikali hiyo wahitishe haraka Mkutano Mkuu wa  kijiji kwa  kuwasomea taarifa za Mapato na Matumizi  na kujadili  masuala mbalimbali ya Maendeleo katika kijiji hicho. " Naagiza Mkutano huo ufanyike mara moja ndani ya kipindi  kisichozidi wiki moja, Wananchi wasomewe Taarifa za mapato na Matumizi , maana ni haki yao yao ya msingi,  na nitaongea na mkurugenzi ili atume haraka sana wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua  na kujiridhisha na Matumizi ya  fedha   katika kijiji hicho na kama itathibitika kuna Matumizi Mabaya ya fedha  wahusika wote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Alisema Bw.Remidius na kuwataka Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, Hata hivyo  amemtaka Mtendaji wa kijiji hicho kujieleza  kwa maandishi kwa nini alifanya udanganyifu wa kuandika Taarifa za Uongo kwa Mkurugenzi kama Muhtasari wa Mkutano uliovunjika  pasipo kumshirikisha Mwenyekiti wa kijiji na Wajumbe  wote wa Serikali ya kijiji hicho huku akifahamu taratibu  zote za kuandika Mihtasari ya vijiji.

Bw.Remidius amewataka Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya kijiji na kusema Maendeleo yanaletwa kwa ushirikiano kati ya Wananchi na Serikali. Hata hivyo Wananchi walionekana kufurahishwa na ujio wa kiongozi huyo na kukubaliana na maamuzi yaliyofikiwa.

Katika hatua nyingine Bw. Remidius ametoa muda wa Wiki moja kwa Wafanyabiashara wote ambao hawana leseni za Biashara  wawe wamelipia leseni hizo kinyume na hapo hatua kali  na msako mkali utafanyika mara moja. " Wapo wafanya biashara  wengi hapa kijijini  ambao hawana Leseni za Biashara , nawapa muda wa wiki moja wawe wamelipia leseni zao na hili ni agizo kwa Tarafa nzima ya Itiso, kinyume na hapo wajiandae kushughulikiwa  kwa mujibu Sheria" Alisema Bw. Remidius

Wakati huo huo Afisa Tarafa huyo  Ameivunja kamati ya Afya ya Zahanati ya kijiji hicho ( Zajilwa) kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kukwamisha ufanisi wa huduma  ya Afya kijijini  hapo   ikiwa  ni pamoja na kukwamisha  juhudi za kijiji hicho katika kutekeleza  Maagizo ya mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Farida Salum Mgomi ambaye pamoja na mambo mengine  amekuwa mstari wa mbele  kuhimiza utoaji bora wa huduma  za Afya na  kuhamasisha Wananchi  kujiunga na Mfuko wa Afya ya jamii (CHF) aidha Bw. Remidius  amegiza kuundwa kwa Kamati mpya ili iendane na kasi  ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.