ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 25, 2015

NAKUTAKIA KILA LA KHERI YA SIKUKUU YA CHRISTMASS NA MWAKA MPYAA


Na Krantz Mwantepele,

“Huku tupo tu tunahangaika na kilimo, tunalima kila mwaka, lakini ukweli ni kwamba kilimo chetu wala hakina faida basi tu bora siku ziende”

Lilikuwa ni jibu toka Alex Jonh maarufu kwa jina la “Mafuriko” mmoja wa wanaharakati na waraghbishi wa kijiji cha Lugunga, kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita baada ya kuulizwa swali kuhusu maendeleo ya kijiji chao na mmoja wa waandishi wa habari za mitandao Ali Masoud maarufu kwa jina la Kipanya.

Kijiji hiki kina wakazi wanakadiriwa kuwa na wakazi 3,685 wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo wadogo. Kilimo kinaajiri karibu 75% ya wakazi wa vijijini. Lakini ni ukweli pia, ni kilimo ambacho bado kinategemea jembe la mkono na mvua na hivyo kuathiri sekta hiyo kwa kiasi kikubwa. Tukiacha hiyo pia upatikanaji wa pembejeo kwa mifumo iliyomo kwenye sera ya kilimo, bado ni changamoto kubwa.

Waraghbishi wengi ni wakulima, ingawa wapo pia walimu, viongozi wa dini, wenyeviti wa vijiji, na watendaji wa kata lakini ukweli unabaki  kwamba wengi wao wanategemea kilimo. Changamoto wanazokutana nazo wakulima ndiyo sababu inayopelekea kilimo kutokuwa cha faida hali inayowakatisha tamaa na kusema bora liende.


Mraghbishi Alex John maarufu kwa jina Mafuriko akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Herieth Makwetta alipotembelea kijijini hapo 



Akielezea masikitiko yake kuhusu hali yetu, mraghbishi Alex John ama Mafuriko anasema:

“Ndugu zangu sisi huku tumesahaulika kabisa, kilimo chetu tunacholima ni kilimo cha bora liende maana hatuna kabisa elimu yoyote hapa kijijini. Kila mtu analima na kupanda anavyojua maana tumeshazoea maisha ya hivi.”

Katika ufafanuzi wake Mafuriko ameendelea kusema kuwa kijiji chao kina ardhi yenye rutuba na inayokubali mazao mengi yakiwemo mahindi, maharage, mpunga na karanga lakini licha ya kuwa na ardhi nzuri kama hiyo bado kilimo hakina faida kwao.

Mchora Katuni Ali Masoud (mwenye miwani) akizungumza na waraghbishi na wananchi wa kijiji cha Lugunga

Lakini ni sababu gani inayowafanya wakose faida katika kilimo chao licha ya kuwa na ardhi nzuri inayokubali zaidi ya mazao ya aina tatu. Hapo ndipo waraghbishi walipoanza kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo.

Akifafanua ukubwa wa tatizo linalowakabili wakulima wa kijiji hapo raia mwamilifu na mraghbishi Gabriel Jonathan anasema:

“Unajua ndugu mwaandishi hapa kijijini tatizo ni moja, asilimia kubwa ni wakulima na wakulima wengi hawana elimu. Unaona, wengi wao wameishia darasa la saba na wengine hawajasoma kabisa, hivyo hata kilimo chao wanalima ili mradi msimu upite hata akilima heka mbili akatoa gunia tano kwake anaona sawa.”

Ni kweli kilimo ni suala la kitaalamu na hivyo kuna uhitaji mkubwa wa ufahamu kwa mkulima, na hapo ndipo serikali inapomwajiri Afisa Kilimo. Ambaye kimsingi ndio mwenye jukumu hilo katika kuhakikisha anawatembelea wakulima na kuwasaidia kitaalamu ili waweze kuzalisha mazao mengi na yenye ubora.

Hali hii iliibua hamu ya kutaka kujua iwapo kijijini hapo yupo Afisa wa Kilimo ama Bwana Shamba kama anavyojulikana na wengi, katika hali ya kutokuridhishwa na kiwango cha huduma anachotoa mtaalamu huyo wa mashamba, mraghbishi Mafuriko alisema,

“Bwana Shamba yupo tena yupo sana lakini hana ushirikiano kabisa na wakulima wa Lugunga, kwanza hakai hapa kijijini. Pili wengine hawamjui kabisa yaani kwa wiki anaweza kuja mara mbili au msimuone mwezi mzima ila mshahara analipwa”

Akiongezea kuhusu upatikanaji wa Afisa huyo Yohana Julius alisema:

“Tunasikia anaishi Masumbwe na anapoishi hatujui ni mtaa gani na wala mimi simjui licha ya kwamba nakaa hapa katikati (Center) hata nikikutana naye bila kuambiwa simjui je mwananchi anayeishi Mahameni itakuwaje”

Mahameni ni kitongoji kilichopo pembeni ya kijiji cha Lugunga ambapo pia bwana Shamba wa kijiji hicho anatakiwa kufika katika kutimiza wajibu wake.

Mraghbishi Gabriel (wa kwanza kushoto) akiwa na wananchi wenzake wa kijiji cha Lugunga, wakisikiliza maswali toka kwa mwandishi


Umbali wa kutoka Masumbwe hadi Lugunga ni kilometa 17 hali inayodhihirisha kuwepo umbali mrefu kati ya anapoishi Afisa kilimo huyo Dickson Silvester na kituo chake cha kazi.

Kukaa tu na kulaumu hakusaidii sana hivyo ni jukumu la waraghbishi kujua nini wanachotakiwa kufanya,  

“Mimi naona hapa tuandamane mpaka ofisi ya Mkurugenzi, yeye ni mwajiri wake na inawezekana akawa hana hata taarifa ya nini kinafanyika huku, alisikika mmoja wa wananchi aliyetambulika kwa jina moja la Hassan.

Katika hatua nyingine wananchi hao wakapaza sauti kwa kumtaka afisa kilimo huyo kurudi kuishi kijijini na kuongeza kuwa kama alikubali kuja kufanya kazi na kupokea mshahara basi akubali kuishi katika kijiji hicho cha Lugunga kama wanavyoishi wananchi alioenda kuwatumikia.

Safari ya kujua ukweli wa kwanini afisa kilimo huyo haishi katika kituo chake cha kazi ilizidi kusonga mbele na ndipo mwandishi wa makala hii alipomtafuta kwa njia ya simu na kufanya naye mahojiano yaliyodumu kwa dakika kumi na tano.

Katika mahojiano hayo afisa kilimo huyo Dickosn Silvester alikiri kuwa yeye ndiye afisa kilimo wa kijiji cha Lugunga na kukanusha taarifa za kuwa haishi katika kituo chake cha kazi.

“Mimi ni afisa kilimo wa Lugunga kweli na ninaishi hapo hapo Lugunga Center aliyekwambia siishi hapo ni nani? Mana huo ni uzushi”, alisikika akisema Dickson kwa njia ya simu wakati akiongea na mwandishi wa makala hii.

Baada ya kupata majibu ambayo hayakuniridhisha kutoka kwa afisa kilimo huyo nilirudi Lugunga kwa njia ya simu na kumtafuta mwenyekiti wa kitongoji cha Lugunga Kati (Center) bwana Mashiba Dioniz ili kupata ukweli yalipo makazi ya afisa kilimo huyo.

“Mimi ndiye mwenyekiti wa kitongoji cha hapa Senta, kwakweli mwandishi huyo afisa kilimo hana makazi hapa mimi nazijua kaya zangu zote, Ila huwa namuona mara moja kwa wiki basi ila kusema anaishi hapa ni uongo kabisa.’ Alisema Bwana Mashiba mwenyekiti wa Lugunga.

Lakini waraghbishi hawa si tu wanajaribu kufuatilia upatikanaji wa huduma za ugani katika kijiji chao, ila wameendelea kutoa elimu kwa wanakajiji wengine wa kijiji hapo. Mfano mmoja ni migogoro baina ya wakulima wenyewe. Na kwa kuwa waraghbishi hawa hawaitishi mikutano ya vijiji mara nyingi wamekuwa wakitumia maeneo ya migogoro kama sehemu yao ya kutolea elimu.

Akifafanua hilo Felix Daudi, mraghbishi mwingine katika kijiji hicho anasema,
“Kuna kesi tunakutana nazo ambazo tunazitumia pia kutoa elimu. Moja ya kesi hizo ni zile na mtu kuacha mifugo yake bila uangalizi na mwishowe inaingia kwenye mashamba ya watu na kuanza kula mazao. Utakuta mtu hajui wapi akapeleke tatizo lake ama akishaikamata mifugo hiyo afanye nayo ni nini,”

Hivyo ni vizuri watendaji wa serikali wakashirikiana na waraghbishi na muda mwingine kuwapatia ujuzi mdogo mdogo. Hii itasaidia kufanikisha shabaha ya Maendeleo kwani pande zote watakuwa wanategemeana. Na si katika hali hii ambayo watu wanashutumiana.  Hivyo ni jukumu letu sote kucheza nafasi zetu katika kusukuma gurudumu la maendeleo.


                        Moja ya mashamba ya mpunga yaliyopo katika kijiji cha Lugunga



                       CHANZO ; MWANAHARAKATI MZALENDO BLOG 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.