ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 31, 2015

BASATA YAMFUNGIA SHILOLE KWA UVUNJIFU WA MAADILI

CHANZO: MWANANCHI
By Louis Kolumbia
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole kujihusisha na shughuli za sanaa kwa muda wa mwaka mmoja.
Mwanamuziki huyo anayejulikana pia kama Shishi Baby amekumbwa na dhahama hiyo baada ya kusambaa kwa picha zinazomuonesha akicheza jukwaani akiwa katika mavazi yanayokinzana na maadili ya Kitanzania akiwa nchini Ubelgiji.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza amezungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo na kusema hatua hiyo imechukuliwa baada ya awali kumpa onyo kwa matukio ya kupanda jukwaani kufanya sanaa akiwa katika mavazi yasiyozingatia maadili ya Kitanzania.
“Awali tulimuonya kwa vitendo hivi, akakiri kosa na kuahidi kwa maandishi kuwa hatarudia kufanya hivyo” alisema na kuongeza: “Hata hivyo, wadau wa muziki watakumbuka alichokifanya nchini Ubelgiji. Lilikuwa tukio la aibu kwake kama msanii, aibu kama mwanamke na aibu kama Mtanzania” alisema.
Amewataka wasanii kujitathimini kabla ya kupanda jukwaani na kuonya kuwa Basata itaendelea kuchukua hatua kama hizo dhidi ya msanii yeyote atakayebainika kuvunja/kukiuka maadili ya nchi. Shilole amekiri kupokea barua kutoka Basata akisema, hivi sasa yuko kwenye majadiliano na mwanasheria wake na kusema anakusudia kukata rufaa kupinga kufungiwa huko. “Mashabiki wangu watulie kwani hii ni changamoto, tunaifanyia kazi kila kitu kitakuwa sawa hivi karibuni” alisema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.