ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 31, 2015

MKANDARASI ACHELEWESHA MRADI WA MAJI SAFI JIMBO LA BUCHOSA WA BILIONI 1.6 APEWA WIKI TATU KUKAMILISHA KAZI HIYO

NA PETER
FABIAN, BUCHOSA (SENGEREMA).
NAIBU Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na KATIBU wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, wamempa muda wa wiki tatu, Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Maji safi Vijijini, akamilishe kazi na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Kampuni ya PET Corporation Ltd, ndiyo Mkandarasi anayejenga mradi wa maji safi wa Lumeya, katika chanzo cha Ziwa Victoria wenye thamani ya sh Bilioni 1.6, ambao sasa umetakiwa kukamilishwa haraka mwezi ujao.

Dk.Tizeba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa,    alisema kwamba awali mradi huo ulitakiwa kukamilika mwaka 2013 lakini kutokana na ‘kusuasua’ kwa Mkandarasi na kuweka sababu za hapa na pale, umesababisha kutokamilika kwa wakati licha ya kulipwa  kiasi cha sh bilioni 1.3.

Tizeba alisema mradi huo utakapokamilika utahudumia zaidi ya wakazi 60,000 wa Vijiji na Vitongoji vya Kata za Nyakarilo, Kalebezo, Nyehunge na Kata mpya ya Bukokwa ambao wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la maji safi salama. 

“Mheshimiwa Katibu wa mkoa, tunataka maji, Aprili 14 mwaka huu lazima yatoke maana mkandarasi huyu amekuwa na sarakasi nyingi, mradi huu ulikuwa ukamilike mwaka 2013 akaongezewa muda hadi Septemba 2014 lakini akashindwa,” alidai Tizeba.

Aidha alifafanua kuwa , hata baada ya kuongezewa muda mwingine na Wizara na Mamlaka ya Maji safi na Mazingira (MWAUWASA) ambao ndiyo wasimamizi hadi Machi 30 mwaka huu, Kampuni ya PET ameshindwa kukamilisha kwa muda huo hivyo nadhani tumpatie siku 21 kutoka juzi (Machi 27) hadi Aprili 15 vinginevyo malipo yake yatazuyiliwa na kuwajibishwa.

Kwa upande wake Katibu Mtaturu akikagua mradi huo,alisema amesikitishwa na sarakasi za Mkandarasi huyo, hivyo ni vyema Serikali ikambana na kutolipwa kiasi kilichobaki hadiatakapokamilisha mradi huo mwezi ujao kutokana na serikali kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kuhakikisha wananchi walioichagua inawapatia huduma.

“Mbunge mimi nitoe ahadi ya kurudi Lumeya Aprili 21 ili kuona kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa ya kupatiwa maji safi na salama wananchi waliokichagua CCM na kuunda serikali na tukikuta Mkandarasi ameshindwa kutekeleza ahadi yake basi tutashauri achukuliwe hatua za kisheria,”alisisitiza.

Mtaturu alisema kwamba Wizara na Mamlaka zinazopewa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo ya wananchi ni vyema wakaweka Wakandarasi wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hizo kwa wakati ili wananchi wapate huduma badala ya kuwapa na kushindwa kuwasimamia na kuasababisha kuchelewesha huduma.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya PET, fundi msimamizi wa mradi huo, Erzeus Joas,  aliahidi viongozi hao kukamilisha kazi ya kufunga mita ya umeme na kulaza bomba la kuchukulia maji kutoka ziwani, Aprili 15 mwaka huu na kuanza kusukuma maji kwa wananchi baada ya siku mbili za majaribio.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.