ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 21, 2014

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AHUTUBIA KATIKA MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA WA LISHE NA VIRUTUBISHO (ICN1) ROME ITALIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia Mkutano wa pili wa Kimataifa kuhusu Lishe na Virutubisho (ICN2) uliofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome, Italia juzi Novemba 19, 2014. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akijadiliana jambo na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania wakati wa mkutano huo wa ICN2 (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Italia, James Nsekela na Msaidizi wa Rais katika Masuala ya Lishe Dkt. Wilbald Lorri. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango Maalum wa Chakula Duniani (WFP) Ethria Cousin (kushoto) na Balozi Wilfred Ngirwa wakati wa mkutano huo wa ICN2, uliofanyika juzi Novemba 19, 2014, Jijini Rome Italy. Picha na OMR
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifuatilia hotuba mbalimbali za viongozi walioshiriki katika Mkutano huo wa ICN2. Kulia ni Mfalme Letsie III wa Lesotho. Picha na OMR
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa FAO Jose Graziano da Silva, wakati alipomtembea ofisini kwake na kufanya naye mazungmzo, juzi Novemba 19, 2014. Kushoto ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid. Picha na OMR
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA KUHUSU LISHE NA VIRUTUBISHO JIJINI ROME, ITALIA NOVEMBA 21, 2014

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal Novemba 19, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa kuhusu Lishe na Virutubisho uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Kilimo na Chakula la 
Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome Italia. 

Mkutano huu umefanyika ikiwa ni miaka 22 baada ya mkutano wa kwanza maarufu kwa jina la ICN1 kufanyika katika jiji la Rome na kuazimia kuwa, upo umuhimu wa kuhakikisha binadamu wanapata Lishe bora yenye virutubisho ili kusadia kujenga afya ya binadamu duniani. Mkutano huu wa pili pia umeandaliwa kwa pamoja na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkutano huo ulifunguliwa na Balozi wa Kudumu wa Italia katika Umoja wa Mataifa Gianni Ghisi aliyesoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Italia Giorgio Napolitano ambapo alifafanua kuwa Rome inawakaribisha wawakilishi wan chi mbalimbali na kwamba inatamani kuona mkutano huu unatoka na majibu ya tatizo la lishe duni kwa watu wa mataifa mbalimbali. 

Katika siku ya ufunguzi pia hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon iliwasilishwa pamoja na uzoefu wa masuala ya Lishe kutoka Italia ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia Paolo Gentiloni aliwasilisha hotuba yake huku akiwakaribisha washiriki wa mkutano huu wa ICN2 katika jiji la Rome na kufafanua kuhusu matarajio ya Italia katika mkutano wa sasa ukilinganisha na ule uliofanyika miaka 22 iliyopita.

Akiwasilisha taarifa ya Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa Maendeleo ambao wamekuwa wakichangia katika sekta za Afya na Kilimo na akafafanua kuwa Tanzania imepiga hatua tangu ICN1 na sasa inahitaji kuona mkutano huu unatoka na maamuzi yanayotekelezeka ili kuwasaidia wananchi wa mataifa mbalimbali hasa watoto na akina mama wajawazito kuwa na uhakika wa lishe bora yenye virutubisho.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto ambavyo vingi vilitokana na lishe duni na kwamba serikali ya Tanzania inaendelea kulipatia msukumo suala la lishe na virutubisho kwa wananchi wenye uhitaji ili kujenga taifa lenye afya na lenye watu wenye uwezo wa kusaidia nguvu zao katika kuleta maendeleo.

Akizungumza siku ya pili ya Mkutano huo Baba Mtakatifu Fransis alisema haki ya chakula bora si tu kuwa imetolewa na Mwenyezi Mungu kwa binadamu bali pia ni haki inayoashiria utu na ambayo haipaswi kutolewa kama zawadi kwa wanadamu. 

Papa Fransis aliendelea kusema kuwa, katika dunia ya sasa masuala ya chakula, lishe na mazingira yametokea kuwaunganisha binadamu wa mataifa yote sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma na akazitaka serikali za dunia kuhakikisha zinapunguza utupaji wa vyakula sambamba na kuongeza mikakati ya kuhakikisha kila mwanadamu anapata lishe bora.

ICN2 inatazama pia kuhakikisha kuwa nchi zinakuwa na mikakati ya kupunguza utapiamlo na kwamba chakula kinachopatikana kiwe kile kilichoboreshwa ama kuongezewa virutubisho ili kusaidia jamii zinazokabiliwa na matatizo kama utapiamlo kuepukana nayo 
na hivyo kuwa na kizazi chenye afya bora na chenye uwezo wa kutumika katika uzalishaji ama katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Dkt. Margareth Chan, Mkurugenzi wa WHO aliueleza mkutano huo kuwa suala la lishe ni mhimili katika kufanya jamii inayoweza kukabiliana na magonjwa huku pia Mkurugenzi wa FAO Jose Graziano da Silva akifafanua kuwa, shirika lake linautumia mkutano huu unaoshirikisha nchi 172 kutoa mwongozo kwa dunia kuhusu jambo hili muhimu katika maisha na hasa sasa ambapo tunaelekea kukamilika kwa Malengo ya Milenia na kuanza malengo mapya.

Katika mkutano huo, licha ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Tanzania pia iliwakilishwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid pamoja na Waziri wa Mifugo Dkt. Titus Kamani sambamba na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dkt. Mahadhi Juma Maalim. 

Sambamba na kuhudhuria mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata fursa ya kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaishi Italia na kufanya nao mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa sambamba na kukutana na Mkurugenzi wa FAO ambaye alionesha furaha yake kuhusu hatua mbalimbali ambazo Tanzania imepitia na kuahidi ushirikiano zaidi katika masuala ya Kilimo. 

Mheshimiwa Makamu wa Rais na ujumbe wake umeondoka kurejea nyumbani Tanzania tayari kuendelea na shughuli nyingine za Kitaifa leo Ijumaa Novemba 21, 2014.
 
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
                       Rome, Italia
                 Novemba 21, 2014

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.