ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 24, 2013

JIJI LA MWANZA LIMEPIGA MARUFUKU KUPANGA BIDHAA NJE YA MADUKA

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza Alifa Hassan Hida (kushoto) akitoa tamko kwa waandishi wa Habari wengine wanaoonekana katika picha ni baadhi ya wadau wa kikosi kazi cha kutekeleza mpango kazi wa kuwapanga wamachinga na kuwaondoa maeneo yasiyoruhusiwa.
Na Peter Fabian
MWANZA.

HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imepiga marufuku na kuagiza wamiliki wa maduka makubwa na madogo kuacha kupanga bidhaa zao nje ya maduka yao na kuwataka wamachinga wote wanaofanya biashara kwenye njia za watembea kwa miguu kando ya barabara za Kenyata na Nyerere kupisha maeneo hayo.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida kwa waandishi wa habari ofisini kwake, alisema kwamba hatua hiyo inafuatia Jiji hilo kutoa muda wa miezi miwili ya kuwataka wafanyabiashara wadogo (Machinga) kufanya biashara zao kwenye maeneo waliyotengewa badala ya kuanza kuzagaa na kupanga bidhaa kiholela.

Mkurugenzi Hida alieleza kuwa kuanzia kesho wataanza kutekeleza sheria ndogo namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 na sheria ndogo ya Usafi wa Mazingira ya mwaka 2010 pamoja na kuendelea kulinda na kulipatia Jiji la Mwanza Hadhi ya Kimataifa itakayoleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kuendelea kuwanufaisha wananchi wake.

“Wananchi wetu kupitia sekta za Utalii,Biashara, Ujenzi wa vitega Uchumi na Uwekezaji katika Jiji letu ili kutuingizia mapato na kuboreshwa mazingira ya upatikanaji huduma kwa wananchi za kiwango cha kitaifa na kimataifa likiwa na mwonekano wenye Hadhi kuendana na kasi ya ukuaji wake.

Hida alifafanua kuwa katika utekelezaji huo ambao unaambatana na Mpango kazi unaozingatia suala la kuwapanga wamachinga ikiwa ni mwendelezo ulioanza tangu mwaka 2007/2008 ili kufanikisha zoezi hili na kuhakikisha Jiji linakuwa kwenye mpangilio mzuri na kila eneo la Mji linatumika kama ilivyokusudiwa.

“Jiji tayari limeisha boresha maeneo ya yaliyotengwa kwa ajili ya masoko ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) kwa kuweka miundombinu mwafaka ya vyoo, maji na vituo vya daladala lakini masoko hayo yamekuwa hayatumiki na kutelekezwa jambo ambalo limewafanya vijana wengi kufanya biashara kiholela katikati ya Mji”alisema.

Alieleza kuwa Jiji lake litaendelea kubaini na kuyaendeleza maeneo yaliyoruhusiwa kwa wafanyabiashara wadogo, kuainisha maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli za biashara za machinga, kuondoa kero nyingine na kuondosha huduma za chakula kwenye vichocholo vya wazi na magenge sehemu mbalimbali zisizoruhusiwa kuwepo huduma hiyo.

“Wamiliki wa maduka tumeisha wapatia muda wa kutosha na kuwatangazia kuwa wanatakiwa kupunguza kero za kutoweka bidhaa zao nje ya maduka, kuweka mapipa ya plasitiki ya kuhifadhia taka pamoja na kuhakikisha mitaro iliyo mbele ya maduka yao haichafuliwi kwa taka ngumu au maji kutuama”alisisitiza

Aliyataja maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli za wafanyabiashra wadogo kuwa ni maeneo yote ya Mzunguko wa Mjini kati  karibu na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) barabara ya Nyerere hadi Nyamhongolo, Pamba kuanzia mzunguko wa mnara wa Nyerere, barabara kuelekea Kanisa Katoliki la Bugando hadi maungiyo ya barabara ya Kenyata.

Barabara zingine alizitaja ni Rwagasore, Lumumba, Karuta, Kenyata, Stesheni ya Reli, Soko kuu la Mjini kati, eneo la stendi ya zamani ya Tanganyika pamoja na maeneo yote ya watembea kwa miguu kwa barabara za Nyerere, Kenyata,Uwanja wa Ndege, Aghakan na kwenye nyumba za ibada za madhehebu mbalimbali.

Mkurugenzi Hida alisema kuwa maeneo yaliyotengwa yataendelea kutumiwa na wafanyabiashara wadogo kuwa ni maeneo ya Mirogo (Community Center), Makoroboi, Uchochoro wa Tanganyika,Stendi ya zamani ya Mkuyuni, barabara ya vitunguu soko kuu, Asante moto, barabara ya Pamba chini (Daraja-White Pub), Market Street na Stendi ya Nyegezi.

“Biashara ya samaki haitaruhusiwa kwenye maeneo hayo na watakao kwenda kinyume na maelekezo ya mpango huo wa kuwapanga wamachinga na wafanyabiashara wamiliki wa maduka makubwa na madogo Jiji litatumia sheria kuhakikisha taratibu hizo zinafuatwa na halitakuwa tayari kukubaliana na wanasiasa kutumia mwanya wa kuwarejesha kwa manufaa ya kujipatia umaarufu”alisisitiza.

Amewataka wananchi na wafanyabiashara wote wakiwemo machinga na mama lishe kutoa  ushirikano kwa wataalamu wa Idara ya Mipango Miji na askari Polisi na wale mgambo wa Jiji wakati wa kuhakikisha mpango wa zoezi hilo unatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili Jiji liendelee kuwa safi na kunyakuwa tena tuzo ikiwemo usafi wa jumla wa kila jumamosi ya kwanza ya kila mwezi

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.