ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 26, 2013

MAAMBUKIZI YA VVU TOKA KWA MAMA MJAMZITO KWENDA KWA MTOTO YANAWEZA KUEPUKWA



MAAMBUKIZI YA VVU  TOKA KWA MAMA  MJAMZITO KWENDA  KWA MTOTO  YANAWEZA KUEPUKWA
Edwin Soko
Mwanza
Tafiti  zinaonyesha  kwamba kuna uwezekano  mkubwa wa mama  mjamzito   kumwambukiza mwanae Virusi  Vya Ukimwi (VVU),  endapo mama  atakuwa  anaishi na Virusi  Vya  ukimwi  kama  hakutakuwa na mipango  mathubuti  ya kimkinga mtoto aliye tumboni kupitia mpango wa kuzuia  maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi toka  kwa  mama mjamzito kwenda  kwa  mtoto(PMTCT). 

Baba ana nafasi ya kumpenda mkewe akiwa mjamzito
Mganga  mkuu wa mkoa wa Mwanza, bwana Valentino  Bangi,  alisema kuwa, virusi vya ukimwi vinaweza kusambazwa kutoka kwa mama mjamzito aliyeambukizwa, hadi kwa mtoto tumboni kwa njia kuu tatu. Njia ya  kwanza  wakati mtoto yungali tumboni mwa mama, ambapo virusi vinaweza kusambaa kutoka kwa mama hadi kwenye nyumba ya uzazi. 

Pili  ni  wakati wa kujifungua, ambapo mtoto anaweza kuingiwa na majimaji ya ukeni au majimaji mengine kutoka kwa mama.  Tatu ni  wakati wa kunyonyesha, ambapo virusi vinaweza kuambukizwa kupitia maziwa anayonyonya mtoto. 
 
Kwa mujibu wa UNICEF, uwezekano wa kumwambukiza mtoto  wakati wa kujifungua ni mkubwa zaidi kama mama ana ujazo mkubwa wa virusi mwilini mwake na kinga yake tayari ni dhaifu. 

Kabla ya mwanamke aliyeambukizwa kupewa usaidizi wowote wa kimatibabu kwanza atafanyiwa uchunguzi wa damu kuona kima cha virusi ndani ya mwili na hali yake ya kinga kwa ujumla. Kama kinga yake itakuwa thabiti na idadi ya virusi ni ndogo mwilini, huenda hatahitaji dawa mpaka kipindi cha mwisho mwisho cha uja uzito yaani baada ya wiki ya 24.

Lakini kama ujazo wa virusi ni mkubwa na kinga mwili ni dhaifu, huenda italazimu kutumia madawa maalumu  ya kupunguza makali ya ukimwi, mapema ili kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto.

Tanzania  ni  moja  kati  ya nchi  zilizo mstari wa mbele  kutekeleza mkakati wa kuzuia  maambukizi   ya  Virusi  Vya  Ukimwi  toka kwa mama  mjamzito kwenda  kwa mtoto(PMTCT) kupitia  huduma zitolewazo na mkakati huo. Hali  hiyo imepelekea  kushuka kwa maambukizi   toka  kwa mama  kwenda  kwa mtoto sanjali na vifo  vya  kina mama wajawazito

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alibainisha kwenye  maadhimisho ya siku  ya  utepe mweupe  yaliyofanyika  duniani kote  na kitaifa  kufanyika mkoani Mwanza     machi 15 mwaka huu   kuwa, vifo  vya kinamama  vinavyotokana  na  uzazi  vimeshuka  kutoka  200 kwa mwaka 2006  hadi  kufikia   vifo 160 kwa mwaka  2012. Hali  hiyo  imsababishwa na kuongezeka  kwa huduma  ya PMTCT.

Nchini Tanzania kwa mujibu wa kituo  cha kuzuia  maambukizi toka  kwa mama mjamzito kwenda  kwa mtoto, kiliainisha takwimu zinaonyesha kuwa, wanawake wajawazito wanaopata huduma ya PMTCT  imeongezeka  toka 34% kwa mwaka 2007 hadi  80% kwa mwaka 2012. Nchini  Kenya  kwa mujibu wa UNICEF pia idadi  imeongezeka toka  56%  kwa  mwaka 2008  hadi 74% kwa mwaka 2008. Nchini Uganda ungezeko ni 27% kwa mwaka 2007 hadi 50% kwa mwaka 2011, kwa mujibu wa ripoti ya wizara  ya  afya ya Uganda.

Dira   ya maendeleo  ya  Taifa 2025 kipengele cha tatu cha  ustawi wa jamii kinasisitiza kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na lengo  la tano la malengo  ya millenia  linasisitiza  kuimarisha huduma za kinamama wajawazito, lengo hilo   zikitekelezwa vyema  ni wazi kwamba hatari ya kumwambukiza mtoto virusi vya ukimwi inaweza kupunguzwa hadi kufikia kati ya asilimia, moja na asilimia mbili tu kama hatua zifuatazo zitazingatiwa. Kupata  matibabu ya  kupambana  na virusi  vya  ukimwi, kuzaa kwa njia  ya  upasuaji na kutonyonyesha kama  mama atabainika kuwa na maambukizi ya virusi  vya ukimwi. 

Sera  ya Taifa  ya  kuthibiti  ukimwi (2001)  katika  lengo  lake  la kwanza inasisitiza juu  ya  kuzuia na  kuenea  kwa ukimwi, hivyo  basi  ni wajibu  baba na jamii  nzima kuzuia  maambukizi  toka kwa mama  kwenda  kwa mtoto ili kuwaokoa watoto wasiambukizwe virusi  hivyo.

Sera ya afya ya Taifa  ya mwaka 2007 moja ya lengo lake kati ya malengo tisa ni kupunguza maradhi kwa wakina mama wajawazito na watoto na kuongeza umri wa kuishi. Huenda  lengo  hili likawa linatia  matumaini kupitia  takwimu, kwani  Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF linabainisha kwamba, maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto yamepungua  kwa  24%  katika nchi ishirini na mbili na nyingi kati ya hizi ni zile ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (2008-2012) umehusisha mchakato wa Ushirikiano wa wadau mbalimbali, kama mashirika  asasi  na watu  binafsi katika kupunguza maambukizi  ya  Virusi  vya  ukimwi.

Shughuli  nyingi za kuzuia  maambukizi  toka  kwa mama  kwenda  kwa  mtoto (PMTCT) nchini Tanzania zimekuwa vikiungwa mkono  na mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupunguza maambukizi  ya  Virusi  Vya  Ukimwi( U.S President’s Emegence Plan for  AIDS Relief ) kupitia shirika  la Engender health  ambalo  umekuwa  ukitoa elimu  kuhusiana na  afya  ya  uzazi wa mpango, kutoa  mafunzo kwa wadau  juu  ya  afya ya uzazi  wa mpango na uzazi  salama.

Mkakati  huo unatukumbusha wajibu wa baba, mama na jamii nzima kushirikiana na kutumia huduma ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) ili kuwakinga watoto wasipate maambukizi hayo. Huduma za  PMTCT  ni pamoja na ushauri na upimaji wa Virusi Vya Ukimwi.  Pia ushauri kuhusu ulishaji wa mtoto aliyezaliwa na mama aliyeambukizwa Virusi Vya Ukimwi, matumizi sahihi ya dawa (ARV) za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi; huduma bora na salama wakati wa kujifungua na ufuatiliaji wa mama na mtoto baada ya kujifungua.

Katika  kujali  hilo Tanzania tarehe 1 Desemba 2012 mheshimiwa  Rais Jakaya  Mrisho Kikwete  alizindua  mpango wa kupunguza  maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda  kwa mtoto kwa mwaka  2012 – 2015. Mpango huo una lengo la kupunguza maambukizi mapya  kwa watoto  na kumfanya  mama kuendelea  kuishi salama.

Kuhakikisha programu ya kuzuia  maambukizi ya Virusi  Vya Ukimwi  toka kwa mama kwenda kwa mtoto  (PMTCT)  inafanikiwa ni lazima hatua zote muhimu zifuatwe, kama kuhudhuria kliniki, kupatikana kwa vipimo,  kukubali kupima,kupata majibu, kupatikana kwa dawa, kukubali dawa, kumeza dawa, dawa kwa mtoto na lishe salama

Hatua mbalimbali za kufuatwa ili kukamilisha programu ya PMTCT)

Makala  haya  yameandaliwa kwa msaada mkubwa  wa sera  ya  Afya  ya Taifa (2007),Sera  ya Taifa ya kuthibiti ukimwi(2001), Dira  ya  maendeleo  ya  Taifa (2005), Mkakati wa pili wa kuthibiti  UKIMWI(2008-2012), Mkakati wa PMCT wa Kenya, Malengo ya Millenia 2015, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania. Mkakati wa kutathimini  hali  ya  PMTCT  Tanzania . Mpango  wa  Uganda wa  kupunguza  maambukizi  mapya  miongoni mwa watoto ifikapo  mwaka 2015 na kuwaweka mama zao  salama.

Kwa maoni na ushauri juu ya makala hii wasiliana na mwandishi 
kupitia Simu No.0754 551 306

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.