ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, February 18, 2013

WANAFUNZI WAKUTWA MAFICHONI KAMA WAHAMIAJI HARAMU KUKWEPA UKAGUZI WA KUSHITUKIZA WA MKUU WA WILAYA


Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi. Amina Masenza akishuhudia mlundikano wa magodoro na hali ya  sehemu wanayolala wavulana wa shule ya Mount Zion kwenye moja ya vyumba vya darasa vilivyotengwa kwa ajili ya kujisitiri.
ZIARA ya kushitukiza iliyofanywa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi. Amina Masenza akiambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kufanya ukaguzi katika shule ya sekondari ya Mount Zion iliyoko ilemela jijini Mwanza imebaini wanafunzi kuishi katika mazingira hatarishi huku uongozi wa shule hiyo ukiwaficha vichakani zaidi ya wanafunzi 50 wa bweni kukwepa ukaguzi. 

Hatua hiyo inafuatia kuwepo taarifa zilizotolewa kwa mkuu huyo na baadhi ya wasamaria wema hali iliyomlazimu mkuu wa wilaya na ujumbe wake kufika shuleni hapo ili kujionea endapo uongozi wa shule hiyo umeboresha kasoro na mapungufu yaliyoonekana baada ya ukaguzi wa awali kufanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita baada ya kutakiwa kuyafanyia kazi mapungufu hayo na Idara ya Afya na Elimu ukaguzi.
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi. Amina Masenza  alishuhudia jinsi hali mbaya kwa vyoo vilivyounganishwa ndani ya bweni njia zikiwa zimebananishwa na masanduku ya bati ya kuhifadhia nguo za wanafunzi bila kuwa na usalama wa kiafya.

Wanafunzi  50 waliobainika kufichwa waumbuliwa.
Hata hivyo jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hizo nalo lilifuatilia na kufanya msako kwenye vichaka vinavyozunguka shule hiyo na kufanikiwa  kuwakuta wanafunzi hao wakiwa wamejificha chini ya ulinzi wa mmoja kati ya waalimu wa shule hiyo kisha kuwaamuru kwenda shuleni ambapo mkuu wa wilaya na ujumbe wake walikuwa wakizungumza na uongozi wa shule na wanafunzi wengine hali iliyo washangaza.
Msafara wa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliojificha na mwalimu wao kukwepa kukutwa wakiwa wamekalia ndoo kwenye msongamano madarasani ukirejeshwa shuleni chini ya uangalizi wa maafisa wa jeshi la polisi nyuma na mbele ya msafara.

Akizungumza huku machozi yakimbubujika kwa uchungu wa hali aliyoishuhudia shuleni hapo Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi. Amina Masenza ameeleza kusikitishwa kwa kitendo hicho na kukilaani vikali akiagiza hatua madhubuti za kisheria kuchukuliwa dhidi ya Mkurugenzi wa shule hiyo….

Msikilize kwa kubofya play..
Hii ndiyo hali halisi ya ukaaji ndani ya darasa hili jeh kwa mpango huu  kuna usalama wa kufanya vyema  kazi za darasani na hatimaye kufaulu kwenye mitiani kihalali?

Shule ya Sekondari ya Mount Zion ina jumla ya vyumba 7 vya madarasa ambavyo ilisajiliwa navyo kuhudumia wanafunzi 160, madarasa yakibaki idadi hiyo, wanafunzi wameongezeka na kuwa 515 hali inayosababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani kiasi cha madarasa mengine kuwa na wanafunzi hadi 119 nao wanafunzi wengine wakilazimika kutumia ndoo kama viti kutokana na uhaba wa mkubwa wa madawati.

Fanya tahtimini ya haraka kwa kila hali ya mwanafunzi huyu wa shule ya Mount Zion anayetumia mapaja yake kama dawati, ndoo kama kiti cha kukalia, chini akiwa na malapa... Ingawa anatabasamu sijui kichwani anawaza nini.... je kwa staili hii tunapaswa kushangaa juu ya matokeo ya kushuka kiwango cha elimu yanayozuka kila miaka?

'Back bencha'

Wanafunzi wanao soma shuleni hapa wengi wanatoka mikoa mbalimbali hapa nchini, hilo lilibainika kupitia mjumbe huyu aliyekuwa akiwauliza wanafunzi hao. Mikoa waliyotaja kutoka ni pamoja na Shinyanga, Mara, Kagera, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Tanga na hata Dar es salaam wapo, kiasi kwamba akawauliza je mlishakalia ndoo au viti vya plastiki hata kwenye shule za msingi mlizotokea? jibu likawa HAPANA

Hifadhi ya masanduku ya wanafunzi wengine waliosongamana kwenye hosteli iliyo mbali kidogo na shuleni hapo.

Nje ya hosteli.

Ni mlundikano wa magodoro chini na hali halisi ya mazingira ya  sehemu wanayolala wavulana wa shule ya Mount Zion kwenye moja ya vyumba vya darasa vilivyotengwa kwaajili ya kujisitiri hali inayoshtusha juu ya uwekaji wa neti kujikinga na malaria.


Ni ndani ya moja ya chumba kidogo cha wasichana ambacho ndani yake kuna matandiko haya  sambamba na  masanduku 13 ikimaanisha ndiyo idadi ya wasichana wanao lala chumbani hiki.


Ndani ya chumba kingine kidogo kwa bweni la wasichana na hii ni style ya kuhifadhi magodoro ya walalaji humu. 

Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya ilemela ikikagua shimo la maji taka ambapo ilibaini bomba kutoka kwenye septik tank kuungwa kwa umbali mrefu hadi sehemu ya wazi na kuyaruhusu maji taka na kinyesi kibichi kumwagika hovyo juu ya ardhi kiasi cha kuweka hali hatarishi kwa afya na urahisi wa mlipuko wa magonjwa kwa wanafuzni na wananchi majirani wa eneo la shule. 

Akiwa amepakizwa kwenye pikipiki kuelekea zahanati ya jeshi iliyo karibu na eneo la shule, mwanafunzi huyu aliyejitambulisha kwa taabu kwa jina la Takiu Kitundu, aliyekuwa hoi akiumwa alikutana njiani na msafara wa kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Bi Amina Masenza, ndipo mkuu huyo akaamuru moja kati ya magari kwenye msafara wake kumuwahisha mwanafunzi huyo hospitali. 
Mwanafunzi mgonjwa akipakiwa kwenye gari la msafara kuwahishwa hospitali.

Dr. Daniel Batane akisoma agizo la ofisi ya Afya wilaya kuifunga mara moja shule hiyo.

Akisoma Ilani ya Kisheria ya kusitisha shughuli za utoaji elimu kwa shule hiyo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo  na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Ilemela, Afisa Afya wa Manispaa ya Wilaya ya Ilemela  Dr.Daniel Batane amesema kuwa kupitia ukaguzi wa kiafya uliofanyika tarehe 13/02/2013 na kufanywa na maofisa Afya kutoka manispaa na kata husika madhaifu mengi yalibainika.

Moja kati ya kasoro zilizoainishwa ni pamoja na mfumo wa maji taka na vyoo ulikutwa ukiwa umejaa hadi kutapisha na pia ni mdogo sana kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi wote 515 wa jinsia zote.

Pia shule hiyo imegundulika kutokuwa na shimo la maji taka kiasi chakuelekeza bomba kutoka kwenye septic tank kwenda kwenye eneo la wazi huku ukimwaga kinyesi kibichi na kusababisha kero kubwa ya harufu kali pamoja na kuweka mazingira hatarishi ya uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko.

Mazingira ya kuhudumia chakula katika shule hiyo yalikutwa hatarishi kiafya, panya wengi wakizagaa kwenye stoo ya chakula sambamba na ushahidi wa panya kukutwa akiwa amefia ndani ya diaba lililokuwa linatumika kuhifadhia maji ya dharura.

Mapungufu mengine yaliyobainishwa ni pamoja na shule hiyo kukosa mabweni rasmi kwa malazi ya wanafunzi zaidi ya kuwa na darasa moja linalotumika kama sehemu ya kulala wanafunzi wavulana.
-Kukosekana kwa vitanda katika vyumba vya wasichana kiasi cha kuwafanya kulala chini kwenye magodoro yaliyochakaa huku hali ya usafi katika vyumba hivyo ikiwa mbaya kutokana na msongamano usiotoa nafasi kwa usafi kufanyika ipasavyo. 

Kufuatia sakata hilo Idara ya Afya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza imetoa agizo la kisheria kuifungia mara moja shule ya Sekondari ya Mount Zion kutokana na kukiuka kanuni za uendeshaji wa shule pamoja na shule hiyo kukithiri kwa uchafu suala ambalo ni kinyume cha sheria ya Afya ya jamii no. 1 ya mwaka 2009.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.