ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, February 27, 2013

MMOJA ANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI WENGINE WAWILI WASAKWA KWA UCHOCHEZI WA VURUGU ZA KIDINI

Kamanda Ernest Mangu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja na kuwasaka wengine wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kueneza na kuchochea vurugu za kidini.


Akizungumza na vyombo vya habari leo katika ukumbi wa mikutano wa jeshi la polisi mkoani Mwanza Kamanda  Ernest Mangu, amemtaja mtu huyo anayeshikiliwa kuwa ni Imam Hamza.

Watuhumiwa wengine wanaosakwa ni pamoja na Shekhe Ilunga Hassan Kapunga, ambaye yuko nchini India akipatiwa matibabu pamoja na Askofu Agustino Mpemba wa kanisa la Tanzania Field Evangelist ambaye vilevile ni Mkurugenzi wa kituo cha redio Kwaneema Fm cha jijini Mwanza ambaye anatajwa kuwa kwa sasa yupo jijini Dar es salaam. Bofya play kumsikiliza Kamanda.



Baadhi ya CD zinazotajwa kuwa mali ya watuhumiwa hao wa makosa ya uchochezi wa kidini.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunakuja kufuatia vurugu zilizotokea Zanzibar na Geita ambapo jeshi hilo liliamua kufanya operesheni maalum kuwasaka watu wanaoeneza uchochezi wa vurugu za kidini. 

Mtuhumiwa Imam Hamza ambaye amekwisha kamatwa na tayari mapema leo amefikishwa mahakamani mkoani  Mwanza anatuhumiwa kuandaa CD inayoitwa 'NDEGE WOTE WALIE AKILIA BUNDI UCHURO' ambapo ndani yake imetajwa kuwa na maudhui ya Uchochezi wa vurugu. 
Kamanda Ernest Mangu akitoa taarifa.
Mwingine ni Shekhe Ilunga Hassan Kapunga anayetuhumiwa kuandaa CD zenye maudhui ya Uchochezi ya kwanza ikiwa na jina la Mauaji ya kinyama ya Shekhe Aboud Rogo wa Mombasa ambayo ameipa jina la 'UNAFIKI KATIKA SENSA' ya pili 'KADHIA YA MUUNGANO WATANGANYIKA NA ZANZIBAR' na ya tatu ameipa jina la 'UADUI WA MAKAFIRI'.

Shekhe Ilunga kwa sasa anatajwa kuwa yuko nchini India ambapo jeshi la polisi nchini kupitia interpol inafanya juhudi ya kumkamata na kumrejesha nchini apate kujibu mashitaka.

Mtuhumiwa wa tatu Askofu Agustino Mpemba wa kanisa la Tanzania Field Evangelist ambaye vilevile ni Mkurugenzi wa kituo cha redio Kwaneema Fm cha jijini Mwanza yeye anatuhumiwa kusambaza CD yenye jina 'INUKA CHINJA ULE' inayotajwa kuwa na maudhui ya kuchochea vurugu huyu anatajwa kuwa kwa sasa yupo jijini Dar es salaam.

Tupe maoni yako

2 comments:

  1. GSENGO MBÖNA HUJAKAMILISHA HABARI?NI KINA NANI? Kosa gani?TUPE HABARI
    MISSANA DHL BUKOBA

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.