ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 29, 2012

MASIHI ANGEKUWA MTANZANIA ANGEKUWA NA UJUMBE GANI?

Jesus Christ Superstar … Carl Anderson as Judas in the 1973 film version. Photograph: Ronald Grant Archive


Anna Mghwira
Kwa takiribani miaka 2000 sasa Waumini wa dini ya Kikristo huadhimisha sikukuu hii ya Krismas ulimwenguni kote. Krismas ni tafsiri fupi ya siku ya kuzaliwa Kristo. Kristo mwenyewe hakuwa Mkristo kwa maana kuwa jina Kristo lilipatikana kwa ujio na mauti yake. Yeye alikua Myahudi wa dini ya Kiyahudi.

Tarehe hasa ya kuzaliwa Kristo haifahamiki ijapo majira yanafahamika na yanatofautiana kati ya desturi mbalimbali za Kikristo. Kwa mfano nchi za magharibi ndizo zinazoadhimisha tarehe 25 Decemba kama siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Kristo Yesu. Desturi ya magharibi inafuata tarehe iliyoandikwa mwaka wa 336 baada ya kuzaliwa Kristo.

Desturi zingine za Kikristo huadhimisha siku hii na kuipa maana tofauti, kwa mfano desturi ya Kiothodox huweka mkazo zaidi katika majira ya kuzaliwa Kristo (epiphany) kuliko siku yenyewe ya kuzaliwa. Hawa pia huhesabu mwaka wao mpya tofauti na mwaka wa kalenda tunaotumia unaotokana na desturi za magharibi. Wao huadhimisha siku za majira ya mwaka mpya mwezi wa nne wa kila mwaka.

Aidha kuna tafsiri mbalimbali juu ya ujio na utambulisho wa Kristo. Kwa jinsi ya desturi za Kiyahudi, alikozaliwa Yesu na ambalo ndilo taifa lake la asili, Kristo yaani Masihi bado hajaja kwa maana kwao masihi ni mfalme wa aina ya kidunia.

Yaani ataonekana kwa macho kama mfalme na si kama alama ya imani. Na si kama mwana wa Mungu kama imani ya Kikristo inavyoelekeza. Baadhi ya Wayahudi pia hawamtambui Yesu kama masihi mpaka leo. Kwa hiyo Kristo wa imani na Kristo wa matendo wanaweza kuwa viumbe viwili tofauti.

Kwa jinsi hii maana ya Krismas inatofautina katika misingi hii. Na kwa sababu hii tafisiri mbalimbali za maana ya Kristo huelekezwa katika maana ya ujio wa Kristo zaidi kuliko katika hali ya kimwili ya kuwa mwana wa Yusufu na Maria.

Kwa hiyo Wakristo huadhimisha siku hii kama ishara ya ujio wa mkombozi wa kiimani zaidi. Maana ya ukombozi wenyewe nayo hutofautiana, wengine wakimtazama Yesu kama Mungu aliyefanyika mwanadamu, wengine wakimtazama kifalsafa na kumpa maana kubwa ya mafunzo ya uadilifu ambayo wakristo wanapaswa kufuata.

Katika mkazo wa mafundisho, kuna mambo mengi yanayohusishwa na ujio wa Kristo ulimwenguni. Tafsiri nyingi zimetawaliwa na desturi za magharibi ambazo kwa kweli hazina uasili na ujio wa Kristo, lakini kama ilivyo katika masuala mengine ya jamii, jamii za awali za magharibi zinaonekana katika historia ya binadamu kuwa na mwamko wa kuchukua mambo na kuyafanyia kazi kwa haraka kuliko jamii zingine na kwa hiyo zinamiliki tafisri za mambo mengi hata yale yasiyokuwa na asili yao.

Kwa hili hatuwezi kuzilaumu jamii hizi au watu binafsi kwa juhudi zao. Tunaweza badala yake kutoa changamoto kwa jamii zingine ulimwenguni na hasa za Afrika ambazo zimekuwa nyuma sana katika kuweka mambo yake katika historia ya ulimwengu na hata kwa mambo yake yenyewe.

Kwa sababu hii tafisri kuu ya kile kinachoitwa Ukristo kwa sehemu kubwa ni desturi ya magharibi na tafsiri yao juu ya dini hii. Ni kwa sehemu inafanana na Uislamu pia ambao una destri kuu ya Kiarabu. Kwa hiyo kwa mfano vita kuu ya maneno na ya silaha kati ya Waarabu na Wazungu ina msingi katika dini zao.

Tukio la septemba 11 la mwaka 2001 lilihitimisha kwa sehemu ugomvi mkali kati ya desturi hizi mbili na mpaka sasa vita vya mashariki ya kati vinajengwa katika msingi wa imani na mali – mafuta kwa upande wa Waarabu na matumizi ya mafuta kwa upande wa Wazungu.

Desturi hizi mbili zinawagusa na kuwaathiri Waafrika kwa namna ambayo si rahisi kujitoa katika makucha ya mabwana hawa wawili: Mzungu na Mwarabu. Kwa hiyo kama kuna ukombozi Mwafrika anahitaji ni kujitoa katika makucha ya hawa kwanza, hata katika tafisri za kiimani.

Kisha kuangalia alikotoka na anakotaka kwenda na atakavyokwenda. Bila ya hivyo ukombozi wa Kikristo unaweza kubaki kuwa ukombozi wa kujua mila na desturi za watu wengine na imani zao, na kamwe usimkomboe Mwafrika. Hili ni kweli ikizingatiwa kuwa ukoloni ulikuja na Ukristo na utumwa ulikuja na Uislam! Tunahitaji kutafakari na kuchukua hatua mapema!

Nitoe mfano wa desturi ya Wakristo kusali wakifumba macho. Utani unakuja kuwa kwa kufundishwa kufumba macho Mwafrika alifumbia macho mambo ya msingi kama rasilimali zake na wakati angali amefunba macho, mzungu akachukua kisha akamtawala!

Kuna ukweli kuwa mila na desturi za Kiafrika hazikuwa na utamaduni wa kufumba macho wakati wa kusali. Makabila yetu mbalimbali huendesha ibada za kimila nuruni, katika mwanga ambapo kila mtu anamwona mwenzake. Aidha dini za asili kadhaa huamini na kuapa kwa jua na mwezi, kwa hiyo kufumba macho hakupo!

Nimewahi kushuhudia mwinjilisti mmoja ambaye alifungua macho wakati wa sala akakuta paka anataka kuchukua samaki waliokuwa wametengwa mezani na bila kujali imani yake na ya kuwa yeye ni kiongozi wa dini, alipoona paka ananyemelea samaki alipiga kelele “ paka anachukua samaki” kwa lugha ya kimila aliyotumia alisema”nyau ahora somba nye”!

Yaani paka anachukua samaki wakati wengine wamefunga macho wakisalia chakula!. Tukio hili lilinifanya nitafakari sana kama kweli imani hii inatokana na kufunga macho ama inatakiwa itokane na kufunga rohoni zaidi ili mtu astahimili kuyafumbia macho mambo ya dunia hii yanayopotosha!

Huu ni upande mmoja wa shilingi, upande wa pili ni kuwa wakoloni Wakristo walipofika na kufundisha kufumba macho ya akili wakati wao wakifumbua na kutumbua, ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo na leo ni vigumu sana kuwatoa katika fahamu zetu, katika mipango ya kujiendeleza na kujikwamua na udhalimu waliouanzisha.

Sheria zetu na umahiri wake msingi wake si zetu kwa kweli, ni mambo ya kuiga na kuigiza! Mwafrika hana desturi ya kumweka mkosaji kizimbani, kumhoji maswali akiwa ametengwa na jamii aliyoikosea. Mwafrika wa asili alitumia njia za matambiko kubaini wakosaji, kisha kuwarejesha ama kuwatenga kwa kuwapeleka mbali na makazi asili ili hayamkini wajifunze na kurejea tabia ya utu.

 Tunahitaji kubadilika! Tunahitaji kufanya kazi ya ziada kujua asili yetu na kuirejesha! Wakati mwingine nimefikiri kuwa pengine turudishe utumwa tena wa jinsi yetu ili hatimae tujikomboe.

Mtihani mkubwa wa imani upo hapo: katika kuyaona mambo mabaya yanayofanywa duniani na yenye mvuto machoni kama vile yanafaa lakini kumbe ndiyo yanayotuangamiza.

Kuzaliwa kwa Kristo ni wito kwa Wakristo kuleta amani, upendo na nuru katika ulimwengu. Ni tafsiri nzuri hata kama haitokani na desturi ambayo ningeitaka. Kwa makala hii niwatakie wasomaji wetu Siku kuu njema na niwape mtihani kufikiri kama masihi angetoka afrika angefananaje na ujumbe wake ungekuwa nini??

Kama masihi huyu angezaliwa leo Tanzania angekuwa na sura na umbo gani?
Angewakilisha kundi gani? 
Angeongea lugha gani? 
Angekuwa na imani gani na angejishughulisha na nini?
Kristo alikuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele. Je tunao uzima huo? 
Yaani maisha bora ya kujitosheleza kusherehekea siku kuu hii na zingine zijazo na tunazoweza kuvumbua?
Mungu atubariki tunapokula na kunywa tusile kama wajinga wasio na imani bali kama werevu wenye hekima! Heri ya krismas kwenu Nyote!

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.