ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 16, 2012

WANAVIKUNDI WAMA WAKUNNWA NA HUDUMA ZA NHIF

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Eugen Mikongoti akizungumza na wanavikundi zaidi ya 400 walio chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati wa akifungua mafunzo kwa wanavikundi hao juu ya utaratibu wa huduma zitolewazoto na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,katika ukumbi wa Mikutano wa Boma,Ilala jijini Dar es Salaam leo.Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Wanawake katika Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA),Tabu Lokoko na katikati ni Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Rehani Athuman.


 Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),Rehani Athumani ambaye ndie mtoa mada mkuu katika mafunzo hayo,akifafanua jambo kwa wanavikundi zaidi ya 400 walio chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati wa semina ya mafunzo kwa wanavikundi hao juu ya utaratibu wa huduma zitolewazoto na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, katika ukumbi wa Mikutano wa Boma,Ilala jijini Dar es Salaam leo.

 

Baadhi ya wanavikundi zaidi ya 400 walio chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakifuatilia kwa makini mafunzo juu ya utaratibu wa huduma zitolewazoto na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, katika ukumbi wa Mikutano wa Boma, Ilala jijini Dar es Salaam leo.

===============================

Na Grace Michael
JUMLA ya wanavikundi 400 walio chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wameridhishwa na utaratibu wa huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hatua iliyowafanya kuahidi kujiunga mara moja ili wawe na uhakika wa kupata matibabu.
Hatua hiyo imefikiwa wakati wa mafunzo yaliyotolewa na NHIF kwa wanavikundi hao Dar es Salaam leo ambapo walielezwa faida wanazoweza kupata kupitia utaratibu wa kujiunga na Mfuko huo.

Kutokana na hatua hiyo, NHIF kwa kushirikiana na WAMA wataandaa utaratibu utakaowawezesha wanavikundi hao kuanza utaratibu huo mara moja ambao utawanufaisha na kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NHIF, Eugen Mikongoti kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika sekta ya afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeendelea kuwa na dhamira ya kuwapatia watanzania wote utaratibu unaoeleweka wa huduma za afya na kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma za matibabu kwa heshima inayostahili.

“Utaratibu wa kupata tiba kwa kadi unao manufaa makubwa kwenu, kwani gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa mno na kama mnavyoelewa ugonjwa haupigi hodi hivyo kwa kuwa na kadi itasaidia kupata matibabu wakati wowote hata kama hamtakuwa na fedha kwa muda huo,” alisema Mikongoti.
Mafunzo ya wanavikundi hao ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotolewa na Mfuko kwa viongozi wa vikundi ambayo yalikuwa na lengo la kuwapa elimu juu ya huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

“Tuko hapa ili tuzungumze fursa na vikwazo vinavyoweza kuukabili mpango wa Bima ya Afya kwa Wajasiriamali,.. dhana hii bado ni ngeni kwa wengi lakini inaweza kuwa na manufaa kwa kuielewa na kuifanyia kazi na sisi kama Mfuko tumejipanga kuhakikisha huduma hii mnaipata kama inavyotakiwa” alisema Mikongoti.

Katika mkutano huo Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Rehani Athumani ambaye aliwasilisha mada iliyohusu huduma za matibabu za uchangiaji kupitia NHIF na CHF ikiwa ni pamoja na manufaa yake.

Rehani aliwaeleza wanavikundi hao kuwa endapo watajiunga na Mfuko huo watapata huduma za matibabu katika hospitali zote za Serikali na za binafsi ambazo zimesajiliwa na Mfuko huo.
Alisema kuwa katika kuhakikisha wanachama wa Bima ya Afya hawakumbani na tatizo la ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma, Mfuko pia umesajili maduka ya dawa ambayo mwanachama anaweza kupata huduma ya dawa kama atakosa huduma hiyo katika kituo cha matibabu alichokwenda.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba kujiunga na Bima ya Afya ili wanufaike na mtandao mkubwa wa huduma za matibabu.

Hata hivyo Rehani hakusita kuwakumbusha wajibu wa kuwa walinzi wa huduma za afya hasa pale wanapoona kasoro za kiutendaji katika vituo vya huduma za matibabu.

Kwa upande wa wanavikundi hao, waliweka wazi msimamo wao kuwa wako tayari kujiunga na utaratibu wa Bima ya Afya ili waweze kunufaika na matibabu hatua ambayo itawapa uhakika zaidi wa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa kuwa mtaji wa masikini ni afya yake mwenyewe.




Kukubali kwa wanachama hao kujiunga na Bima ya Afya ni moja ya mafanikio makubwa ya WAMA ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha inawaunganisha wajasiliamali hao na watoa huduma kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.