ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 1, 2012

KOMEDI WA MWANZA, DAR KUWASHA MOTO CCM KIRUMBA JUMAMOSI, KINGWENDU NDANI

HOMA ya pambano la soka la wasanii wa vichekesho vya luninga ‘komedi’ wa kutoka mkoani Dar es Salaam na jijini Mwanza ‘Rock City’, imepanda baada ya mastaa hao kutambiana kuwa kesho Jumamosi katika Uwanja wa CCM Kirumba patachimbika.
Kingwendu
Tayari wachekeshaji wa Dar es Salaam wamewasili Mwanza kwa mchezo huo maalumu wenye lengo la kutoa burudani, kumaliza ubishi wa nani zaidi kati yao na kujenga ushirikiano kwa wasanii hao.

Mechi hiyo imekuwa gumzo kubwa katika jiji la Mwanza na mikoa ya jirani ya Kanda ya Ziwa, baada ya wachekeshaji Kingwendu na Bambo kuwasili mkoani humo na kutamba kupitia vyombo vya habari kwamba, wamekwenda kutafuta ushindi katika mchezo huo.

Kwa mujibu wa mratibu wa mechi hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Brayance Promortes, Pearson Samwel, maandalizi yote yamekamilika na kinachosubiriwa siku ya mchezo ili kumaliza ubishi uliotawala wa komedi wa Dar es Salaam na Mwanza kina nani wanaweza kusakata soka.

“Tunashukuru tumekamilisha maandalizi yote na wasanii wote wamefanya mazoezi kwa ajili ya kucheza soka kwa dakika 90 na wanatazamia kutoa ushindani mkubwa kati yao,” alisema Samwel kutoka Mwanza.

Alisema kuwa viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh 2,000 mzunguko na sh. 5,000 katika jukwaa kuu na mpaka jana walikuwa wanakamilisha taratibu za mwisho kupata mgeni rasmi.

Wasanii kutoka Dar es Salaam watakaoshuka ndani ya CCM Kirumba siku hiyo ni Kingwendu, Sharo Milionea, Mboto, Senga, Pembe, Bambo, Mtanga, Mau, Ringo na Chilly, Defender, Zimwi, Muhogo Mchungu, Masele, Erick, Kiuno na Hawa.

Timu ya wachekeshaji wa Mkoa wa Mwanza inaundwa na Babu Mkombe,Sharobaro wa Kihaya, Mchele, Chugu, Ngosha, Brother K, Mama Brandina, Msimbe wa ukweli,Okech Okech, Kafuku Kaukananga, Mzee Dude, Itagata, Malapulapu, Choko na Tengambili.

Wasanii wengine watakuwepo siku hiyo ni Tatu Mkate wa Arusha, Avodia Tolu, Mrefu kwenda chini na Jully Tax, ambao wamepania kuwafunga wachekeshaji wenzao wa Dar es Salaam.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.