ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, October 27, 2011

SITTA - SIGOMBEI URAIS 2015

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema hana ndoto ya kuwania urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.Kauli hiyo ya kwanza ya Sitta ambaye pia ni kada wa CCM, imekuja wakati ambao kuna mpasuko mkubwa ndani ya chama chake hicho ambao unahusishwa na mbio za urais wa 2015, huku yeye akitajwa kuwa mmoja wa wenye nia ya kushiriki mbio hizo.

Kauli yake imeingia katika orodha ya kauli za makada wengine kadhaa ambazo zimetikisa siasa za CCM huku nyingi zikiwa na sura ya mvutano tena zikitolea nje ya vikao rasmi vya chama hicho tawala nchini.

Hata hivyo, juzi usiku akijibu swali kama ana ndoto ya kuwania urais au la, Sitta alisema: "Hapana! Sina ndoto ya kuwania urais kwa sasa, wapo vijana watajitokeza, wapo wazuri, tutawaunga mkono tu".

Sitta alifafanua kwamba matumaini yake mwaka 2015 watakuwapo wagombea wenye uwezo wakiwemo vijana, na kuongeza, "wale wazalendo wenye maadili wataungwa mkono".

Ingawa, Sitta amesema hana ndoto ya kuwania urais kwa sasa, lakini amekuwa akitajwa kama mmoja wa watu wanaoutaka baada ya Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015, kutokana na nguvu zake kubwa alizojijengea kwa umma.

Sitta aliweza kujipatia umaarufu mkubwa kisiasa baada ya kuongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa ambalo alikuwa na kauli mbiu yake ya Bunge la Kasi na Viwango.

Kuhusu chuki ya watu aliowaita mafisadi, Sitta alisema watuhumiwa hao walifanya mbinu mbalimbali kuhakikisha hafanikiwa katika malengo ya kurejea kwenye uspika wa Bunge la Kumi kwani waliendesha hujumu nzito dhidi yake.

Sitta aliwatuhumu watu hao akisema: "Mafisadi hawanitaki, wananichukia wako tayari hata kuniua".


CHANZO: Mwananchi

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.