ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 16, 2011

KIKAO CHA MKUU WA MKOA UONGOZI WA JIJI PAMOJA NA WAFANYABIASHARA WAKUBWA NA WAMACHINGA -16/07/2011

Kikao cha mkuu wa mkoa, uongozi wa jiji pamoja na wafanyabiashara wakubwa na wadogo kimefanyika leo katika ukumbi wa ofisi za jiji mkoani Mwanza.

Suala kubwa lililojadiliwa ndani ya kikao hicho ni vurugu za wamachinga zilizotokea hivi karibuni na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa, upotevu wa mali na hasara ya mapato kwa serikali kwani kwa siku nzima hakuna biashara iliyofunguliwa, hivyo kikao hicho kilikaa kujadili nini chanzo na ufumbuzi.

Huku akitolea mfano moja ya taarifa iliyotoka katika gazeti la Mzawa ikieleza kiini cha vurugu hizo na kuwataja Mh. Wenje (mbunge) na Mh. Manyerere (Meya wa jiji) kuwa ndiyo waliochochea vurugu hizo baada ya kutajwa na mwenyekiti wa kamati ya mipango miji na Mazingira ya Halmashauri ya jiji la Mwanza Bw. Henry Matata (Diwani CHADEMA), Mfanyabiashara Mohamed Msukuma amesikitishwa sana na kitendo cha wanasiasa kuendekeza propaganda kwa maslahi yao na kutaka uchunguzi ufanyike na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe juu yao.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika mahojiano maalum Bw. Matata amenukuliwa akiwaonya baadhi ya wanasiasa waliochochea vurugu hizo kwa maslahi yao binafsi nakutaka wakamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kukomesha vurugu za mara kwa mara zinaziofanywa na wafanyabiashara wadogo wadogo jijini hapa. Pia kiongozi huyo ameshangazwa na namna ya vyombo vya dola vinavoshindwa kuwachukulia hatua baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kila kukicha. Amewalaumu viongozi hao kwa kuiyumbisha Halmashauri ya jiji kwa wao kugeuka kuwa watoa idhini na vibali bila kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa.

Ndani ya kikao hicho Bw. Matata alithibitisha kauli yake kwa kusema kuwa "Dawa ya ugonjwa ni kujua tatizo nami nipo hapa kwaajili ya Wananchi na siyo marafiki toka chama changu, ni ukweli ulio wazi Meya wa jiji na Mbunge wanapaswa kuheshimu maamuzi sahihi yanayoafikiwa vikaoni kwa ajili ya maslahi ya jiji la Mwanza badala ya kusaka umaarufu, Meya na Mbunge wanapaswa kuacha kuingilia mambo kwa kujifanya wao kuwa watendaji wakati sheria zipo"

Akijibu hoja na shutuma dhidi ya jiji kwa upande wake mkurugenzi wa jiji Bw. Wilson Kabwe amesema kuwa siyo kwamba wamachinga hawajapewa sehemu kwaajili ya kufanya biashara bali kuna maeneo rasmi yaliyoruhusiwa kwa wao kufanya biashara tena kwa muda ulioafikiwa na si eneo hilo la msikiti lililoleta vurugu kwa wachache kulivamia, ambalo kimsingi linahitajika kuwa wazi kwaajili ya wanaotoka na kuingia ibadani.

Amani hailindwi bali amani hujengwa na kutunzwa, matokeo ya wamachinga ni Indiketa tu za mabaya yanayokuja hivyo tusipojipanga basi tumekwisha! Tutakuja kuteketea wote!

Watu wa daladala, wamachinga, pikipiki na wengine wote, wako mjini kwa haki tatizo ni kutozingatia sheria nao watumishi wa serikali na wananchi wametetereka katika kuzisimamia sheria, hilo limebainika ndani ya kikao hicho hii leo.

Viongozi wa jiji washirikiane na viongozi wa wamachinga kwa taarifa, nchi ya China imeweza kukabiliana na suala kama hili mara baada ya kuwashirikisha wadau husika kwa taratibu na kanuni.

Kwa kujifunza mapungufu yaliyotokea kwa utaratibu na ujenzi wa MACHINGA COMPLEX DAR, tayari halmashauri ya jiji la Mwanza imepanga kujenga soko maalum katikati ya jiji kwa ajili ya wamachinga na wafanyabiashara wengine yaani 'ONE TRADE CENTRE' litakalojumuisha biashara aina zote.

Sambamba na wamachinga hao kuamriwa kutoka maeneo wasiyo ruhusiwa, pia imegundulika kuwa machafuko hayo ya mara kwa mara yamesababishwa na migogoro ya kiuongozi baina ya viongozi waliopo ndani ya Shirika la wamachinga Mwanza waliojitenga ambao nao wana uongozi wao uliotoa maamuzi ya kugawa maeneo ya biashara bila kuzingatia kanuni zilizowekwa ikiwa ni pamoja na ugawaji wa eneo hilo lililoleta vurugu.

Mkuu wa mkoa amewaagiza viongozi hao kuitisha mkutano haraka iwezekanavyo utakao husisha pande zote wakubaliane kuja na maamuzi ya pamoja yatakayowasilishwa kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.