ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, April 21, 2011

WALIOTAKA 'KUMUUA' DK. CHEGENI KIZIMBANI

Watuhumiwa wa mtandao wa kula njama kutaka kumuua kwa risasi aliyekuwa mbunge wa zamani wa Jimbo la Busega, wilayani Magu, mkoani Mwanza, Dk. Raphael Masunga Chegeni, wamefikishwa mahakamani kisha kusomewa mashitaka yanayowakabili.WATUHUMIWA WAKIINGIA KIZIMBANI.
Watuhumiwa hao kwa pamoja walipandishwa jana katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, mbele ya Hakimu Angerus Lumisha, wakikabiliwa na kesi ya jinai namba 113/2011, ambapo wakiwa katika chumba cha mahakama mawakili wao walianza kujibizana na hakimu kwa kutumia lugha ya Kiingereza kwa takriban dakika 15 hivi.

Katika kesi hiyo ya mauaji, Dismas Zacharia Kamani ni mtuhumiwa namba moja wa kesi hiyo ya mauaji, Erasto Casmil ni mtuhumiwa namba mbili, Queen Joseph Bogohe ni mtuhumiwa namba tatu na Ellen Bogohe, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Siasa ya CCM mkoani Mwanza na diwani wa zamani wa viti maalumu Kata ya Kisesa wilayani Magu, mkoani hapa, ni mtuhumiwa namba nne wa kesi hiyo ya jinai.

Ilielezwa mbele ya mahakama kwamba, Aprili 13 mwaka huu, kwa pamoja watuhumiwa hao walikula njama za kutaka kumuua Dk. Chegeni. ALIYE PICHANI KULIA-->

Paschary Malungu ndiye mwanasheria wa upande wa mlalamikaji (Jamhuri), wa kesi hiyo, huku watuhumiwa Ellen Bogohe na Queen Joseph Bogohe wakitetewa na wanasheria wao wawili wa kujitegemea, Mathew Nkanda na Raurian Vedasto.

Mbele ya mahakama ilidaiwa kwamba watuhumiwa wote kwa pamoja walikula njama kutaka kuua kinyume cha kifungu cha sheria namba 215 ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.


MJUMBE KAMATI YA SIASA CCM ALIYETANGULIA NA QUEEN.
Watuhumiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 6 mchana, walipandishwa kizimbani majira ya saa 9:25 alasiri, na wakiwa kizimbani, yalitokea majibizano kati ya hakimu na mwanasheria mmoja ambapo majibizano hayo yalifanyika kwa Kiingereza kuhusiana na mwenendo wa sheria za nchi, hasa zile za mauaji (jinai).

Baada ya majibizano hayo, Hakimu Malungu alimhoji mtuhumiwa mmoja baada ya mwingine akianzia kwa mtuhumiwa namba nne, Ellen Bogohe, Queen Joseph Bogohe, Erasto Casmil na Dismas Zacharia Kamani, iwapo wanataka kesi yao iendeshwe kwa Kiingereza ama Kiswahili, lakini watuhumiwa wote kwa pamoja walisema iendeshwe kwa Kiswahili.

Upande wa utetezi uliiomba mahakama hiyo kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao kwa madai kuwa hawawezi kuharibu upelelezi unaoendelea na kwamba bado haijafahamika iwapo kesi ya wateja wao itasikilizwa na Mahakama Kuu ama la, lakini hakimu alitupilia mbali ombi hilo. Badala yake aliamuru watuhumiwa kurudishwa rumande hadi leo saa 5 asubuhi mahakama itakapoamua kesi hiyo isikilizwe na mahakama ipi.

Tupe maoni yako

1 comments:

  1. "Mmmhhh, Kwahiyo jamaa aliyepo madarakani ameshindwa kabisa kutafuta mbinu zingine za kuhakikisha jamaa haishiki tena hiyo nafasi na badala yake anafikia uamuzi wa kutaka kuchakachua uhai.?!!! Mbona mapema sana?"

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.