ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 5, 2011

HABARI ZILIZOVUNJIKA MUDA HUU KUTOKA ARUSHA...!

Kufuatia harakati za maandamano ya CHADEMA kupigwa stop na hatimaye vurugu kuzuka na kupelekea watu kadhaa kujeruhiwa vibaya. Wanachama wa Chadema wanaelekea kituo cha polisi cha Arusha viongozi wao wanakoshikiliwa. Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya.UWANJA WA NATION MILLING, UNGALIMITED ARUSHA MAHALA PA MKUTANO.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na wabunge wengine wawili wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, ni miongoni mwa watu kadhaa waliotiwa mbaroni jana na polisi wa mkoani Arusha, kutokana na vurugu za maandamano.

Wengine waliokamatwa ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema. Katika vurugu hizo, pia walikamatwa mke wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema na makada mbali mbali wa chama hicho, huku baadhi yao wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi.

Vurugu zilitokana na kukamatwa wabunge hao ambao walikuwa wakiongoza maandamano ya amani,yaliyoazia katika hoteli ya Mount Meru majira ya saa saba mchana.

Viongozi wa Chadema pamoja na wafuasi wa chama hicho walikusanyika katika hoteli hiyo majira ya saa sita mchana na kuanza maandamano kulekea viwanja vya NMC ulikokuwa umepengwa kufanyika mkutano mkubwa wa hadhara ambao ulikuwa umepengwa kuhutubiwa na Dk Slaa.

Wakiwa katika eneo liitwalo Kwa Dk Mohamed barabara kuu ya Arusha-Moshi, polisi waliwazingira viongozi wa chadema waliokuwa wakiongoza maandamano na kuanza kuwapiga, kuwakamata kisha kuwatupa kwenye magari yao.

Katika purukushani hizo, Mbowe aliangukia kwenye mtaro pembezoni mwa barabara kutokana na kuzongwa na polisi, huku mke wa Dk Slaa, Josephin akishushwa kwenye gari na kupigwa sambamba na polisi hao kuvunja vioo vya gari la mbunge wa viti maalum, Grace Kiwelu.

Hadi jana jioni wabunge hao na wananchi wengine walikuwa bado wakishikiliwa na polisi na habari zaidi zinadai kwamba walikuwa wakiendelea kuhojiwa.

Kituo kikuu cha polisi cha mjini Arusha kilikuwa kimewekewa ulinzi mkali kutokana na hofu ya kuvamiwa na wananchi kwa lengo la kuwakombioa watuhumiwa waliokamatwa.

Barabara ya Makongoro ilifungwa kutokana na vurugu hizo, huku mamia ya wakazi wa Arusha wakiwa pembezoni mwa barabara wakifuatilia vurugu hizo.

Akizungumza kabla ya kukamatwa, Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema aliwaomba polisi kutambua maandamano yao ni halali kutokana na kuwa na kibali na kwamba yalikuwa ya amani.

Polisi walikuwa wakiongozwa na maafisa kadhaa wa jeshi hilo, Mkuu wa upelelezi mkoa wa Arusha, Mkuu wa usalama wa barabarani wa mkoa, Amir Konja Mkuu wa polisi wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeki na maafisa kadhaa toka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.


HABARI KWA HISANI YA Mwananchi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.