ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 24, 2010

TANZANIA TENA GIZANI.

TANESCO YATANGAZA MGAO WA UMEME NCHI NZIMA.
SHIRIKA la Umeme (Tanesco) juzi lilitangaza mgawo mpya na mkubwa wa nishati hiyo ambao utavifanya viwanda, maduka, ofisi na makazi kukosa umeme kwa kati ya masaa sita hadi 12 kwa muda wa mwezi mzima.Tangazo hilo la mgawo ambalo limekuja katika kipindi ambacho mjadala wa jenereta za kampuni ya Dowans ukiwa umeibuka tena, linatarajiwa kuongeza gharama za maisha kutokana na ukweli kuwa viwanda vingi vitalazimika kutumia jenereta katika uzalishaji licha ya Tanesco kutangaza kuwa vitapewa umeme nyakati za mchana. Tangazo la Tanesco limetolewa wakati kukiwa na ahadi kemkem za kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ikiwa imeliruhusu shirika hilo la umma kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 18.5. "Mgawo utahusisha mikoa yote iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa isipokuwa mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Lindi na Mtwara." Kwa mujibu wa Badra Masoud, mgawo wa sasa umetokana na upungufu wa umeme uliojitokeza baada ya moja ya visima vinavyozalisha gesi vya kampuni ya Pan African Energy, kuzimwa. Alisema kisima hicho kinachotoa gesi kimezimwa kwa ajili ya kukifanyia matengenezo ya kawaida, hivyo kusababisha upungufu wa megawati 40 za umeme zinazokwenda katika gridi ya taifa. Pan African Energy ni kampuni ambayo inachimba gesi hiyo eneo la Songo Songo, Kilwa na baadaye husafishwa na kusafirishwa na kampuni ya Songas ambayo huzalisha umeme wa megawati 180 eneo la Ubungo na kuiuzia Tanesco. Kwa mujibu wa makubaliano, Songas hutakiwa kuzalisha umeme kwa kiwango kilicho kwenye mkataba na ni jukumu la Tanesco kuutumia umeme huo wa gesi kulingana na mahitaji yake au kutoutumia. Tanesco huilipa Songas hata pale inapokuwa haitumii umeme wa kampuni hiyo.Badra alisema kuwa kiwango hicho cha upungufu wa umeme kinaweza kuongezeka hadi kufikia megawati 120 jambo alilosema likitokea, shirikma hilo litazidisha mgawo.
Alieleza kuwa mgawo huo utaanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika baadhi ya maeneo huku maeneo yaliyopata umeme katika muda huo yakiukosa kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku mara tatu kwa wiki. Kwa mujibu wa Badra, ratiba ya mgawo huo zitatangazwa katika magazeti na vyombo vingine vya habari. Hata hivyo, alisema baadhi ya maeneo hayatakumbwa na mgawo huo akitaja baadhi kuwa ni hospitali, pampu za maji, migodi na viwandani ambako alisema vitakosa umeme usiku ili mchana viendelee kuzalisha. Alisema kuwa maeneo yanayopata umeme kutoka transoma ya Kipawa hawatakumbwa na mgawo huo, kutokana na kukamilika kwa matengenezo yake. Akizungumzia siku kuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, Badra alisema Tanesco itajitahidi kuhakikisha wananchi wanasherehekea siku hizo bila kukosa umeme huku akiwaomba radhi kwa mgawo huo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.