ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, August 27, 2010

KENYA YAONGOZWA KWA KATIBA MPYA.

MWAI KIBAKI AKITIA SAINI.

Kenya imeandika historia mpya ya utawala nchini humo kwa kuidhinisha katiba mpya, iliyotungwa na wananchi wenyewe, baada ya ile iliyokuwa ikiitumia kabla ya kupata uhuru wake mwaka 1963.

Rais Mwai Kibaki, aliwaongoza maelefu ya raia wake walioshuhudia akitia saini katiba mpya ya nchi hiyo katika sherehe zilizofanyika viwanja vya Bustani ya Uhuru mjini Nairobi siku ya Ijumaa.

Baada ya kutia saini nakala sita za katiba hiyo, wimbo wa taifa la Kenya ukapigwa na kufuatiwa na mizinga 21 ya heshima.

Rais Kibaki, Waziri Mkuu Raila Odinga, Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, Spika wa bunge na wabunge wamekula kiapo cha kuilinda, kuitetea, na kuiheshimu katiba hiyo mpya kwa manufaa na ustawi wa taifa la Kenya na watu wake.

MWELEKEO MPYA.
Katiba hiyo imepangwa kuzuia aina yoyote ya vurugu kama zile zilizofuatia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, wakati zaidi ya watu elfu moja waliuawa kutokana na mgogoro wa kupinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Kibaki.

Pia ina udhibiti mkubwa kuhusu madaraka ya rais, na inatoa madaraka kwa serikali za majimbo na kuwaongezea uhuru wananchi.


UTATA.
Miongoni mwa viongozi wa mataifa ya kigeni waliohudhuria ni Rais Omar Al Bashir wa nchi jirani ya Sudan ambaye anatakiwa na mahakama ya kimataifa inayoshughulikia uhalifu wa kivita, kwa tuhuma za kuendesha mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Kufika kwake katika sherehe hizo kumeonekana kuyakera baadhi ya makundi yakiwemo ya haki za binadamu na mabalozi hususan kutoka nchi za magharibi.

Afisa mkuu wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya, Muthoni Wanyeki ni miongoni mwa watu walioishutumu serikali ya Rais Kibaki kumwaalika kiongozi huyo wa Sudan.

Wanyeki amekaririwa akisema " Ni aibu kwa Wakenya ambao waliuchagua utawala ambao unatakiwa kusimamia hazi za binadamu na badala yake wamekiuka hilo, jambo ambalo dhahiri linaashiria mwisho wa kuwaadhibu wakosaji si tu nchini Kenya bali katika ukanda huu wa Afrika.

Amesema, "Si mwanzo mwema wa utekelezaji wa katiba mpya. Katiba Mpya inabainisha wazi kuwa tunawajibika kutekeleza mikataba yote ya kimataifa ambayo tumeridhia, ikimaanisha tunalazimika kushirikiana na mahakama hiyo ya ICC."

Hata hivyo, serikali ya Kenya imetetea uamuzi wake wa kumwalika Rais Omar al Bashir, kuhudhuria sherehe hizo.

Akizungumzia wito wa kuitaka Kenya kumkamata Rais huyo wa Sudan, Waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Moses Wetangula, amekaririwa akisema, Rais Bashir yupo nchini hapa kwa mwaliko uliofanywa na serikali ya Kenya kwa jirani zake wote kuwaomba kuhudhuria tukio hili la kihistoria.

Bw Wetangula amesema, "Kenya haijavunja sheria yoyote na ni nchi huru, hivyo ina haki ya kumwalika yeyote inayetaka aje hapa nchini."

Kuhusu kutomkamata Rais Bashir kama ambavyo nchi wanachama wa mahakama ya ICC wanatakiwa kutekeleza agizo la mahakama hiyo, Wetangula amesema, "Huwezi kumdhuru au kumfedhehesha mgeni wako, huu si utaratibu, desturi na maadili ya Kiafrika."


KWA HISANI YA BBC SWAHILI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.