ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, July 6, 2010

FIESTA jipanguse ..2010 MWANZA ndiyo MWISHO.

JIJI LA MWANZA MAHALA AMBAPO WAKAZI WAKE WAMEPEWA DHAMANA YA KUHITIMISHA MAADHIMISHO YA FIESTA 2010.

*FIESTA 2010*
Tamasha la kumi la burudani na michezo na sanaa nchini Tanzania, linalojulikana zaidi kwa jina la Fiesta limewadia, msimu unaanza tarehe 7 mwezi Julai ambapo utakuwa ni msisimko wa burudani kwa mwezi mzima, huku wasanii wakitembelea baadhi ya mikoa ya Tanzania yenye msisimko wa sanaa kujumuika na mashabiki wa sanaa, na kuonesha kazi zao.

Kwa mwaka huu wa 2010, Fiesta imepewa msemo wa Jipanguse, ikiwa na mlengo wa kuhamasisha vijana, kuachana na tabia ya kulalamika kuhusiana na matatizo wanayokutana nayo katika maisha yao ya kila siku, na badala yake wachukulie matatizo hayo kama ni sawa na kuanguka, wajipanguse na kuendelea na safari ya maisha..

Kauli mbiu hii inamsisitiza kijana wa kitanzania kuachana na habari za kuhubiri matatizo yake huku akiomba msaada wa kuyatatua wakati akitumainiwa kama mjenzi wa Taifa, kupitia burudani kijana anaelimishwa kuhubiri jinsi ya kuutumia ujana wake kukabiliana na ugumu wa Taifa akiwa kama nguzo ya Taifa.


Mikoa nane ya Tanzania itajipangusa kiburudani na tamasha hili ambalo hufanyika mara moja tu kila mwaka huku mwaka huu mikoa ya Arusha na Moshi ikitarajia kupata ugenni kutoka Burundi ambapo mwanamuziki anayesifika kwa tungo za mahaba mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya, anayejulikana kwa jina la Kidumu, anatarajiwa kufanya maonesho mawili makali na kulipa tamasha hili mtazamo mtofauti mwaka huu.

Katika kuanzia, tarehe 7.07.2010 katika viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro, kuanzia saa nne asubuhi patakuwa na mambo, yakiwemo yale ya mbio za mikokoteni, kukimbia na magunia, mbio za baiskeli za walemavu na za kawaida na baada ya hapo, wanamuziki mahiri wanaoiendesha fani ya muziki wa kizazi kipya nchini watatarajiwa kupanda jukwaani kuonesha sanaa yao kwa mashabiki wa muziki wa mkoa huo.

Hii itakuwa ni kabla ya kuelekea katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambapo matamasha ya mikoa hii yatafanyika tarehe 9 na 10.

Tamasha hilo litazunguka katika mikoa 8 ambayo ni Morogoro, Arusha, Moshi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar, Musoma na Mwanza.

Ratiba kamili inasema, baada ya Morogoro tarehe 7, tarehe 9 ni Matongee Club Arusha na tarehe 10, kazi itakuwa mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Moshi katika ukumbi wa La Liga.

Baada ya hapo Ijumaa ya tarehe 16 Julai, kazi itakuwa Royal Village ambapo wasanii hawa watafanya onesho kali la usiku na kisha kesho yake, yaani mchana wa tarehe 17 Julai, uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma tamasha litafanyika kwa ajili ya familia.

Tarehe 24 Julai, safari ya kuelekea mkoani Tanga uwanja wa mkwakwani na kama ilivyokuwa katika ufunguzi, mashindano mbali mbali, na kisha burudani kwa wakazi wa mkoa wa Tanga.

Mwisho wa mwezi sasa, ndipo tamasha kubwa kwa ajili ya mji mkubwa, huku msanii wa kimataifa na uwakilishi wa kutosha wa Afrika Mashariki utaonekana. Jiji la Dar es Salaam na vitogoji vywake litajipangusa na kuwa safi na kisha litajitupa katika ama Viwanja vya Leaders au vya Posta Kijitonyama, mtafahamishwa zaidi kuhusiana na hili kadri tunavyoendelea.

Baada ya hapo safari ya kuelekea visiwani Zanzibar itaanza na huko burudani itaangushwa pembezoni mwa bustani ya Forodhani, ndani ya ukumbi wa Ngome Kongwe. Wakazi wa Zanzibar wataipata burudani hii kwa masaa yasiyozidi saba, na kisha wasanii watarudi Dar es Salaam kujiandaa na safari ya Musoma.

Huko Tamasha litafanyika Musoma Hotel siku ya Ijumaa ya tarehe 6, na msanii mwenyeji wa huko atakuwa ni Beatrice Moses, mwana Hip Hop ambaye ni zao la shindano la Bongo Star Search 2009.

Tamasha litafungwa mkoani Mwanza, ambapo tarehe 7 mwezi wa nane, ndani ya ukumbi wa Yatch, kutakuwa na patashika nguo kuchanika, na kisha kujipangusa na burudani hii ya muziki, na siiku inayofuata, kazi itamalizikia CCM kirumba ambapo mashindano ya michezo na burudani ya muziki vitaunguruma.

Tamasha la mwaka huu linakuja likiwa na wasanii wapatao 30 ambao ni Diamond, Belle 9, Hussein Machozi, Baby J, Offside Trick, Chege& Temba, Shaa, Juma Nature, Dully Sykes, Barnaba, Amini, Linah, Godzilla, Joh Makini, Roma, Kiki Wa Pili, Young Dee, Fid Q, Mwana Fa, Mataaluma, JCB, Tip Top, Mwasiti, Pina na Beatrice.

Fiesta Jipanguse ya 2010, inakujia kwa hisani kubwa ya Serengeti Breweries Limited, Precision Air, Prime Time Promotions, Kitangoma Magazine, Mradi wa kuzuia Malaria wa Zinduka, na Clouds FM.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.